Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Timu za Amerika Kusini zimekuwa
zikihusishwa na matukio ya vurugu katika baadhi ya michezo ya soka, hali ambayo
mara kadhaa imekuwa ikivuta mjadala kuhusu nidhamu ya wachezaji, viongozi na
namna ushindani unavyosimamiwa ndani na nje ya uwanja.
Matukio ya kugombana, kushambuliana na
wakati mwingine mashabiki kuingia uwanjani yamekuwa sehemu ya matukio
yanayoripotiwa katika baadhi ya mashindano ya ukanda huo. Hata hivyo, si kila
mchezo unaofanyika Amerika Kusini huishia kwa vurugu.
Tukio la novemba 1, 2026, nchini Brazil
limeongeza sura nyingine katika mjadala huo baada ya mchezo wa nusu fainali ya
michuano ya vijana chini ya miaka 20 (U20), kati ya Uberlândia na Mamoré,
kuacha historia ya kutolewa kwa kadi nyekundu 51.
Katika mchezo huo uliokuwa ukiendelea kwa
ushindani, Mamoré ilikuwa mbele kwa mabao 3-1 kabla ya hali kubadilika na
kugeuka kuwa vurugu kufuatia mchezaji Davi Fernandes Bittencourt kufanya ishara
zilizowachokoza watu waliokuwa kwenye benchi la Uberlândia wakati wa
kushangilia bao.
Hali hiyo ilimfanya kocha wa makipa wa
Uberlândia, Paulo Sergio Dias dos Santos, kwenda kumkabili mchezaji huyo. Tukio
hilo likasababisha mapigano yaliyowahusisha wachezaji na viongozi wa benchi la
ufundi wa timu zote mbili.
Kutokana na hali hiyo, mwamuzi alitoa jumla
ya kadi nyekundu 51, ambapo wachezaji 43 na maafisa wanane wa benchi la ufundi
walionyeshwa kadi hizo. Mchezo huo haukuweza kuendelea kutokana na vurugu
zilizotokea.
Idadi hiyo imezidi rekodi ya awali ya kadi
nyekundu 36 zilizotolewa katika mchezo mmoja kati ya Atlético Claypole na
Victoriano Arenas nchini Argentina, Februari 27, 2011.
Matukio haya yanaonyesha namna ambavyo
ushindani unapokosa mipaka ya nidhamu unaweza kuathiri mchezo na kugeuza uwanja
wa soka kuwa eneo la mapambano.
Pamoja na ushindani mkubwa unaotambulisha
soka la Amerika Kusini, tukio la Brazil linaibua tena swali kuhusu wajibu wa
vyama vya soka, waamuzi, makocha na wachezaji katika kuhakikisha matokeo ya
mchezo hayawi sababu ya kuvunja misingi ya nidhamu.
Mwisho wa yote, soka ni mchezo wa
ushindani, lakini ushindani huo unapaswa kubaki ndani ya sheria za mchezo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment