Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Idadi ya wachezaji waliowahi kuitumikia Ligi Kuu Tanzania Bara, baadae kuondoka kwenda kucheza nje ya nchi hatimaye kurejea tena inaendelea kuongezeka. Miongoni mwao ni winga raia wa Msumbiji, Luis Miquissone, ambaye sasa amerejea nchini kwa ajili ya kuitumikia Singida Black Stars akitokea Al Ahly Benghazi ya Libya.
Miquissone si mgeni katika soka la Tanzania, kwani aliwahi kuitumikia Simba SC katika vipindi viwili tofauti ambapo Kwa mara ya kwanza alijiunga na klabu hiyo Januari 2020 akitokea UD Songo ya Msumbiji, ambapo alicheza hadi Agosti 2021 kabla ya kusajiliwa na Al Ahly ya Misri.
Baada ya kuitumikia Al Ahly, alikwenda Abha Club ya Saudi Arabia kwa mkopo mwaka 2022, kabla ya kurejea tena Simba mwaka 2023, Hata hivyo safari yake ya pili Msimbazi ilidumu hadi mwaka 2024, alipoondoka na kurejea UD Songo ya Msumbiji.
Mwaka 2026 alijiunga na Al Ahly Benghazi ya Libya, kabla ya kupata nafasi nyingine ya kurejea katika Ligi Kuu Tanzania Bara kupitia Singida Black Stars.
Kurejea kwa Miquissone ni sehemu ya mwenendo ambao umekuwa ukijitokeza kwa wachezaji mbalimbali waliowahi kucheza Tanzania, kwenda nje ya nchi na baadaye kurudi. Miongoni mwao ni Clatous Chama, Aziz Ki, Himid Mao, Elias Maguli, sadio kanute, Selemani Mwalim na wengine Wengi.
Hali hii inazua swali Je, wachezaji hawa wanashindwa kupata mafanikio katika ligi wanazokwenda kucheza nje ya nchi?
Jibu si lazima liwe ndiyo kwani Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kumfanya mchezaji aamue kurejea Tanzania, zikiwemo maslahi, mazingira ya maisha, utamaduni na nafasi ya kucheza.
Ikumbukwe kuwa, Selemani Mwalimu aliwahi kueleza kuvutiwa kwake na maisha ya Tanzania kutokana na mazingira na utamaduni wa nchi hii, Ukarimu wa Watanzania, kutokuwepo kwa ubaguzi kwa wageni, utamaduni wa vyakula na gharama za maisha ni miongoni mwa mambo yanayoweza kumfanya mchezaji wa kigeni ajisikie vizuri anapokuwa nchini alisema hayo wakati akihojiwa kuhusu hali ya maisha nchini Morocco alipo kuwa akiiitumukia Wydad Casablanca.
Hivyo, kurejea kwa wachezaji hawa hakumaanishi moja kwa moja kuwa wameshindwa katika nchi walizokwenda, hii inaweza pia kuwa ni uamuzi unaotokana na mazingira wanayoyakuta, maslahi wanayopata na namna wanavyothaminiwa.
Kwa ujumla, kurejea kwa wachezaji waliowahi kucheza nje ya nchi kunaonyesha kuwa Tanzania bado ni sehemu inayoweza kuwapa nafasi ya kuendeleza vipaji vyao na maisha yao ya soka, Ligi Kuu Tanzania Bara si njia ya wachezaji kwenda nje pekee, bali pia ni sehemu ambayo baadhi yao wanaamua kurejea na kuendelea na safari zao katika soka.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment