Nyota apagawa na furaha, asahau kuhusu kadi nyekundu


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Baada ya kipindi cha michezo tisa mfululizo bila ushindi katika mashindano yote, hatimaye klabu ya Manchester United imepata ushindi wake wa kwanza kwa kuifunga AS Roma mabao 3-2 katika mchezo wa UEFA Champions League uliopigwa kwenye dimba la Old Trafford.

Katika mchezo huo, United ilijikuta nyuma kwa mabao 2-0, hali iliyozua maswali kuhusu uwezekano wa kuendelea kupitia kipindi kigumu cha kukosa matokeo chanya, hata hivyo, dakika ya 58 Bruno Fernandes aliifungia United bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti, kabla ya dakika ya 83 na 86 kuleta mabadiliko ya matokeo baada ya Matheus Cunha kufunga mabao yaliyoiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Hata hivyo, dakika ya 90+1 Cunha alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kufanya madhambi na kuondolewa uwanjani kwa Kadi nyekundu baada ya awali kuonyeshwa kadi ya njano kwa kosa la kuvua jezi wakati akishangilia.


 Baada ya kuonyeshwa kadi hiyo, Cunha alitakiwa kuondoka katika eneo la kuchezea na eneo la benchi la ufundi kwa mujibu wa sheria za soka , badala ya kuondoka moja kwa moja kuelekea vyumbani, mchezaji huyo alichukua muda na kwenda kukaa jukwaani pamoja na mashabiki, akifuatilia dakika zilizokuwa zimebaki za mchezo.

Baadaye aliondoka kuelekea vyumbani, lakini baada ya kipenga cha mwisho alirejea tena uwanjani kuungana na wachezaji wenzake kusherehekea ushindi huo.

Kitendo hicho kilimfanya kocha wa Manchester United, Michael Carrick, kumtaka kurejea vyumbani ili kuepusha uwezekano wa kukabiliwa na hatua nyingine za kinidhamu kutokana na kutofuata maelekezo baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu.


Inaonekana furaha ya kuiona Manchester United ikivunja mfululizo wa michezo tisa bila ushindi ilimfanya Cunha asahau kwa muda kuwa alikuwa ametolewa kwa kadi nyekundu, Furaha ya ushindi ilikuwa kubwa, lakini haikuondoa ukweli kwamba alikuwa bado chini ya adhabu ya kutoshiriki mchezo huo.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.





0/Post a Comment/Comments