Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Katika ulimwengu wa sasa, soka limekuwa zaidi ya mchezo wa burudani, limegeuka kuwa sekta ya kiuchumi inayoweza kutoa ajira, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya nchi. Hata hivyo, kwa sehemu kubwa ya nchi za Afrika, soka bado halijapewa nafasi inayostahili kama sekta inayoweza kuwa chanzo cha ajira kwa vijana.
Ni jambo la kawaida kuona vijana wengi wenye vipaji vya soka barani Afrika wakifanya juhudi kubwa ili kupata nafasi ya kucheza katika ligi za Ulaya, Wengi wao wamefanya kucheza Ulaya ni ndoto inayohusishwa na kupata kipato kizuri, kutambulika kimataifa na kujenga maisha kupitia soka.
Lakini hapa ndipo tunapopaswa kujiuliza, kwa nini mchezaji kutoka Afrika aone mafanikio yake yanategemea kucheza Ulaya, wakati mchezaji kutoka Ulaya anaweza kujenga maisha yake ya soka akiwa kwenye ligi za kwao bila kulazimika kuja Afrika kutafuta mafanikio hayo?
Hali hii inaonesha tofauti iliyopo katika uwekezaji wa soka kati ya bara la Afrika na Ulaya. Ligi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto za kiuchumi, miundombinu, usimamizi na maslahi ya wachezaji. Matokeo yake, baadhi ya wachezaji wanapopata nafasi ya kwenda Ulaya huondoka bila kusita, kwa sababu wanaamini huko ndiko watakapopata mazingira bora ya kufanya kazi yao.
Hata hivyo, hali hii inaweza kubadilika ikiwa nchi za Afrika zitaamua kuwekeza katika sekta ya michezo kwa kuweka mifumo itakayowezesha ligi zao kuwa na ushindani na kutoa maslahi yanayolingana na thamani ya wachezaji.
Ni muhimu nchi za Afrika kuboresha miundombinu ya michezo, kuimarisha usimamizi wa ligi, kuvutia wawekezaji na kuhakikisha vilabu vina uwezo wa kulipa mishahara inayokidhi mahitaji ya wachezaji, hatua hizi zinaweza kuongeza ushindani wa ndani na kufanya soka kuwa ajira yenye uhakika kwa vijana wengi kwani rasimali zipo ila mipango ndio inatakiwa kwenye sekta ya michezo.
Mfano wa kuangalia ni Saudi Arabia, nchi iliyopo barani Asia. Kupitia uwekezaji katika soka, nchi hiyo imefanikiwa kuvutia wachezaji wanaotambulika duniani, akiwemo Cristiano Ronaldo, ambaye alijiunga na Al Nassr mwaka 2023.
Hatua hiyo imeonesha namna uwekezaji, maslahi ya wachezaji na mikakati ya kukuza ligi vinavyoweza kubadilisha taswira ya mashindano ya ndani na kuongeza mvuto wake kimataifa.
Ikiwa Saudi Arabia imeweza kutumia uwekezaji kuvutia wachezaji wakubwa, kwa nini nchi za Afrika zisijifunze kutoka katika mfano huo na kuanza kujenga ligi zenye uwezo wa kukuza vipaji vya wachezaji na maslahi Yao?
Hapa hoja si kuzuia wachezaji wa Afrika kwenda Ulaya bali ni kuhakikisha wanapochagua kuondoka, wanafanya hivyo kwa ajili ya changamoto mpya za kisoka na si kwa sababu ligi za nyumbani haziwezi kuwapa maisha bora.
Aidha, uwekezaji katika michezo hauishii kwa wachezaji pekee pia Sekta hii inaweza kutengeneza ajira kwa makocha, waamuzi, waandishi wa habari, wapiga picha, wataalamu wa afya za michezo, wachambuzi, mameneja na watu wanaojihusisha na biashara zinazozunguka michezo.
Hivyo, serikali za Afrika zinapaswa kuanza kuitazama sekta ya michezo kama eneo la uwekezaji na si burudani pekee. Kuweka bajeti, kutengeneza sera rafiki kwa wawekezaji na kushirikiana na sekta binafsi kunaweza kufungua milango ya ajira kwa maelfu ya vijana.
Ni wakati wa Afrika kuamka na kuwekeza katika michezo , tusijenge mazingira ambayo mafanikio ya mwanasoka wa Afrika yanapimwa kwa uwezo wake wa kupata timu Ulaya pekee, bali tujenge mazingira ambayo hata kucheza katika ligi za Afrika kunaweza kumpa mchezaji maisha bora.
Afrika ina vipaji, ina vijana na ina wapenzi wa soka, Kinachohitajika sasa ni uwekezaji, mipango na utashi wa kisiasa ili rasilimali hizo ziweze kuleta manufaa ya kiuchumi kwa bara Hilo.
Maendeleo ya soka la Afrika hayapaswi kuishia katika kuzalisha wachezaji wa kwenda Ulaya, bali pia kujenga ligi zitakazoweza kuwapa vijana wake maisha kupitia vipaji vyao wakiwa nyumbani.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.





Post a Comment