Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
"Wareno wenzangu, muda umefika mimi kuirejesha jezi namba saba kwenu sikuwaahi kudhani ni yangu pekee, Kwa miaka 23 nilipata bahati ya kuibeba na kuipigania katika viwanja mbalimbali duniani. Leo muda umefika kuikabidhi kwa kizazi kijacho."
Hayo ni maneno ya nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, akitangaza uamuzi wa kutundika daruga katika soka la kimataifa baada ya kuitumikia nchi yake kwa miaka 23.
Uamuzi huo unaufanya mwaka 2026 kuwa sehemu ya historia ya soka duniani, mwaka ambao mashabiki wanaanza kuaga kizazi cha wachezaji waliotawala mchezo huo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Kabla ya Ronaldo, Neymar Jr alianza kuaga safari yake na timu ya taifa ya Brazil, akifuatiwa na Lionel Messi wa Argentina. Sasa Ronaldo anakuwa jina jingine kubwa katika kizazi hicho kinachofikia mwisho wa safari yake katika soka la kimataifa na wote wakihitimisha safari Yao baada ya kombe la Dunia 2026.
Kwa upande wa Ronaldo, safari yake na Ureno ilianza Agosti 2003 akiwa na umri wa miaka 18, Tangu wakati huo amekuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho, akishiriki mashindano mbalimbali na kuiongoza nchi yake kutwaa mataji ya Euro 2016 pamoja na UEFA Nations League mwaka 2019 na 2025.
Katika kipindi cha miaka 23, Ronaldo ameweka rekodi ya kucheza michezo 234 na kufunga mabao 146, takwimu zinazomfanya kuwa mfungaji bora katika historia ya soka la kimataifa kwa upande wa wanaume.
Ni vigumu kufikiria mashindano ya kimataifa bila uwepo wa majina kama Messi, Ronaldo na Neymar. Kwa miaka mingi, mashabiki wamekuwa wakifuatilia ushindani wao, hasa kati ya Messi na Ronaldo, huku Neymar akiwa sehemu ya kizazi hicho kilichotoa burudani kwa wapenzi wa soka.
Kuondoka kwao katika timu za taifa kunafunga ukurasa wa ushindani uliodumu kwa miaka mingi, huku kizazi kipya kikitarajiwa kuchukua nafasi ya nyota hao katika mashindano yajayo.
Hata hivyo, kwa Ronaldo, huu si mwisho wa safari yake ya soka kwa ujumla, bali ni mwisho wa kuitumikia Ureno akiwa mchezaji wa kimataifa kwa sasa bado anaendelea na majukumu yake ya soka la klabu yake ya Al nasry ya Saudi Arabia.
Kwa namna hiyo, mwaka 2026 hautakumbukwa kwa matokeo na mataji pekee, bali pia kwa kuwa mwisho wa kizazi kilichoweka alama kubwa katika historia ya soka duniani.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.
.


Post a Comment