MICHEZO KAZINI NI SEHEMU YA KUJENGA AFYA BORA NA USTAWI WA WATUMISHI



Adeladius Makwega


Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa – Dodoma.

 

Picha unayoiona hapo juu inawaonesha baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, jijini Dodoma, wakishiriki mazoezi ya viungo. Novemba 10, 2026, Mwanakwetu alipata fursa ya kualikwa na kushiriki mazoezi hayo pamoja na watumishi hao.

Kwa kusema kweli, Mwanakwetu alikuwa miongoni mwa watu wasiokuwa na mwamko wa kushiriki mazoezi haya, licha ya kuwa amekuwa akialikwa mara kwa mara. Hata hivyo, siku hiyo aliamua kubadilika, akakubali mwaliko na kushiriki mazoezi hayo. Baada ya zoezi kukamilika, alipata pia nafasi ya kuwapiga picha watumishi walioshiriki.

 

Katika kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mazoezi hayo, Mwanakwetu alielezwa kuwa:

 

“Watumishi wa Umma wanatakiwa kushiriki mazoezi ya viungo mara mbili kwa wiki, siku za Jumanne na Alhamisi. Hili ni takwa la miongozo na kanunu kwa mujibu wa OSHA, taasisi inayosimamia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.Pia  hata  Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, 2003

(The Occupational Health and Safety Act, No. 5 of 2003), Ilitungwa mwaka 2003 na kwa sasa inapatikana pia kama Sura ya 297 (Chapter 297) katika toleo lililofanyiwa mapitio.”




 

Mtoa maelezo alifafanua kuwa taasisi za umma zinatakiwa kuzingatia utekelezaji wa agizo hilo na kwamba utekelezaji wake hufuatiliwa. Aliongeza kuwa mazoezi ya viungo yana mchango mkubwa katika kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la juu la damu na magonjwa mengine yanayohusiana na mtindo wa maisha.

Siku hiyo, akiwa katika eneo lake la kazi, Mwanakwetu alishuhudia utaratibu mzima wa maandalizi na utekelezaji wa mazoezi hayo.

Watumishi waliokuwepo kazini waliendelea na majukumu yao hadi saa 9:30 alasiri. Baada ya hapo, walielekea vyumbani kubadilisha mavazi ya kazi na kuvaa sare za michezo. Saa 10:00 kamili alasiri, watumishi wakiwa wamevalia sare zao za michezo, walikusanyika uwanjani tayari kwa mazoezi.

 

Mazoezi hayo yaliongozwa na Ndugu Antony Kasili, ambaye ni Afisa Kumbukumbu. Alianza kwa kuwaongoza wenzake kufanya mazoezi mepesi ya viungo, kisha wakaendelea na mazoezi ya kasi ya wastani na hatimaye mazoezi yenye uzito zaidi. Zoezi zima lilikamilika saa 11:00 jioni.

 

Katika kufuatilia namna muda ulivyotumika, Mwanakwetu alibaini kuwa dakika 60 za mazoezi ziligawanywa kwa utaratibu ufuatao:

“Dakika 10 za mazoezi mepesi ya kujiandaa.Dakika 10 za mazoezi ya kasi ya wastani.Dakika 20 za mazoezi yenye uzito zaidi.Dakika 10 za mazoezi mepesi ya kutuliza mwili.Dakika 10 za mazungumzo, matangazo na mapumziko.”

 

Baada ya kukamilika kwa mazoezi, watumishi walielekea kwenye mabafu kwa ajili ya kuoga, kubadilisha mavazi ya michezo na kuvaa nguo zao za kawaida kabla ya kurejea majumbani.

 

Katika kufanya utafiti wake mdogo kuhusu masuala ya michezo na mazoezi ya viungo mahali pa kazi, Mwanakwetu amebaini kuwa suala hili linahitaji kupewa uzito unaostahili na taasisi zote.

 

Kama ambavyo taasisi zinavyotakiwa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kuzimia moto, pamoja na kuwapatia watumishi mafunzo ya namna ya kukabiliana na majanga ya moto, vivyo hivyo, masuala ya usalama, afya na ustawi wa watumishi yanapaswa kupewa kipaumbele, ikiwemo kuweka mazingira rafiki ya kufanya mazoezi kazini.

Hata hivyo, Mwanakwetu amebaini kuwa taasisi nyingi bado hazijawa na utaratibu madhubuti wa kutekeleza mazoezi haya. Katika baadhi ya taasisi ambazo mazoezi hufanyika, bado kuna changamoto zinazoweza kuwakatisha tamaa watumishi kushiriki.

Changamoto hizo ni pamoja na:

“Miundombinu duni ya michezo: Baadhi ya taasisi hazina maeneo na vifaa vinavyokidhi mahitaji ya kufanya mazoezi.Uhaba wa viwanja bora: Kukosekana kwa viwanja vinavyofaa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za michezo na mazoezi.Ukosefu wa mabafu ya kutosha: Baadhi ya maeneo ya kazi hayana mabafu yanayowawezesha watumishi kuoga baada ya mazoezi.Uhaba wa vifaa vya huduma ya kwanza: Kukosekana kwa vifaa muhimu vya kutoa huduma ya kwanza endapo mtumishi atapata changamoto ya kiafya wakati wa mazoezi.Ukosefu wa usimamizi wa kitaalamu wa afya: Baadhi ya taasisi hazina utaratibu mzuri wa kuhakikisha uwepo wa msaada wa kitaalamu wa afya pale unapohitajika wakati wa michezo.”

 

Changamoto hizi ni miongoni mwa vikwazo vinavyoweza kupunguza ushiriki wa watumishi katika mazoezi ya viungo mahali pa kazi. Hivyo, ni muhimu kwa taasisi husika kuzitafutia ufumbuzi ili kuweka mazingira salama na rafiki kwa watumishi.

 

Pamoja na changamoto hizo, viongozi wa Serikali wameendelea kusisitiza umuhimu wa taasisi kuhakikisha watumishi wanashiriki katika mazoezi ya viungo na michezo mahali pa kazi.

Kwa mfano, mwezi Agosti 2026, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ndugu Juma Mkomi, alisisitiza kuwa kila taasisi inapaswa kuzingatia ushiriki wa watumishi katika mazoezi hayo na kuhakikisha uwepo wa mazingira bora yanayowezesha shughuli hizo kufanyika.

Msisitizo huu unaonesha umuhimu wa michezo na mazoezi ya viungo katika kujenga afya bora, kuongeza uchangamfu, kuimarisha mshikamano miongoni mwa watumishi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

 

Mwanakwetu upo?

Ni wakati sasa kwa kila taasisi kuchukua hatua kuhakikisha mazoezi ya viungo yanafanyika kwa utaratibu unaofaa, huku watumishi wakipewa mazingira bora, vifaa na usimamizi unaohitajika.

Aidha, kila mtumishi anapaswa kutambua kuwa afya njema ni msingi muhimu wa utendaji bora kazini. Tusisubiri mpaka tuanze kukabiliwa na changamoto za kiafya ndipo tutambue umuhimu wa mazoezi.

Kumbuka: MICHEZO KAZINI NI SEHEMU YA KUJENGA AFYA BORA NA USTAWI WA WATUMISHI.

Nakutakia siku njema!

makwadeladius@gmail.com
0717649257

















 

 

 

0/Post a Comment/Comments