Mawazo ya wanafunzi yalivyo tengeneza timu tishio Ulaya


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mwezi Novemba una nafasi katika historia ya klabu ya Juventus ya Italia, baada ya kuanzishwa rasmi Novemba 1, 1897, na kundi la wanafunzi wa shule ya upili ya Massimo d'Azeglio iliyopo jijini Turin.

Wanafunzi hao waliamua kuanzisha klabu ya soka wakiwa na lengo la kushiriki katika mchezo huo ambapo Walichagua jina la Juventus lililo tokana na neno la Kilatini lenye maana ya ujana.

Kwa hiyo, Juventus ni miongoni mwa klabu ambazo historia yake ilianzia katika mawazo ya vijana waliokuwa bado katika hatua za masomo, Miaka iliyofuata, klabu hiyo iliendelea kukua na kuanza kushiriki katika mashindano ya soka nchini Italia.

Mwaka 1905, Juventus ilifanikiwa kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa ligi ya Italia. Awali, timu hiyo ilikuwa ikitumia jezi za rangi ya waridi, kabla ya kuanza kutumia rangi nyeusi na nyeupe mwaka 1903, ambazo zimeendelea kuwa sehemu ya utamaduni ake hadi hivi Leo.


Katika safari yake ya miaka 129, Juventus imekusanya mataji 36 ya Serie A, mataji 15 ya Coppa Italia na mataji tisa ya Supercoppa Italiana.

Katika mashindano ya Ulaya, klabu hiyo imetwaa mataji mawili ya UEFA Champions League, mataji matatu ya UEFA Cup na taji moja la UEFA Cup Winners Cup.

Historia ya Juventus inatoa somo kwa wanafunzi kwamba mawazo yanayozaliwa katika mazingira ya shule yanaweza kukua na kuwa taasisi zinazotambulika kimataifa, Kundi la wanafunzi lililoanzisha klabu hiyo mwaka 1897 liliweka msingi wa historia ambayo imeendelea kwa zaidi ya karne moja.


Novemba 1 ya kila mwaka inabaki kuwa kumbukumbu ya siku ambayo kundi la wanafunzi lilianza safari ya kuunda klabu ambayo leo inajulikana kama Juventus.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments