Kocha aadhibiwa kwa kosa lisilo lake


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Licha ya kuwepo kwa vikao na majadiliano kuhusu kumfuta kazi Michael Carrick aliyekuwa kocha wa Manchester United, bado aliendelea kwenda mazoezini na kukutana na wachezaji, jambo linaloonyesha dhamira na upendo aliokuwa nao kwa klabu hiyo licha ya hali iliyokuwa ikiendelea.

Kufukuzwa kwa Carrick katika nafasi hiyo ni uamuzi ambao haukupaswa kufanyika kwa wakati huu, licha ya matokeo mabovu ambayo timu ilikuwa ikiyapata. Kocha huyo alihitaji kupewa muda zaidi kwa sababuu United ilikuwa bado katika mchakato wa kujenga kikosi na kurejesha ushindani wake.

Kwa namna nyingine, hili ni kama jumba bovu lililomuangukia Carrick. Kwa hakika, amechukuliwa kama mbuzi wa kafara kutokana na matatizo ambayo hayahusiani na benchi la ufundi pekee.

Hoja kubwa iliyokuwepo ni kushindwa kwa uongozi wa klabu kukamilisha baadhi ya matakwa ya kocha katika usajili wa wachezaji, hata hivyo, timu iliposhindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa, Carrick ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwajibishwa kwa kuondolewa katika nafasi yake.


Kwa takwimu zake tangu alipopewa jukumu la kuiongoza United Januari 2026, Carrick ameweza kushinda michezo 11 kati ya 16 ya kwanza, akikusanya alama 36 na kuifikisha timu hiyo nafasi ya tatu katika Ligi Kuu England msimu wa 2025/26.

Mafanikio hayo yaliifanya Manchester United kurejea katika michuano ya UEFA Champions League msimu uliofuata, baada ya kukaa nje ya mashindano hayo kwa msimu mmoja.

Hata hivyo, msimu wa 2026/27 matokeo yalibadilika, ambapo United ilianza kupata matokeo yasiyoridhisha na kushindwa kuendeleza kiwango kilichoonekana katika kipindi cha awali cha uongozi wake.

Pamoja na changamoto hizo, swali linabaki kuwa je, Carrick alipewa muda wa kutosha kujenga kikosi ambacho kingeweza kushindana, au amebeba lawama za matatizo ambayo yanahitaji ufumbuzi kutoka kwa uongozi mzima wa United?

Ni wazi kuwa kocha anapaswa kuwajibika kwa matokeo ya timu, lakini mafanikio ya klabu hayawezi kujengwa na benchi la ufundi pekee bila ushirikiano wa uongozi katika kukamilisha mahitaji ya kikosi.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments