Adeladius Makwega – MBAGALA
Novemba 12, 2026, Mwanakwetu alitembelea ukurasa wa Facebook wa mwanahabari na Afisa Habari mkongwe nchini Tanzania, aliyebobea katika sekta ya umma, rasilimaliwatu na utawala, ndugu James Katubuka. Akiwa hapo, alikutana na picha moja nzuri iliyokuwa na maelezo yafuatayo:
“Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, akifuatilia kwa makini wasilisho kuhusu masuala ya rasilimaliwatu katika Mkutano wa 11 wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS HRMNET), unaoendelea leo, Novemba 11, 2026, Zanzibar.”
Mwanakwetu alivutiwa sana na kupendezwa na namna Naibu Katibu Mkuu huyo alivyovaa, akasema moyoni:
“Lo salale bin Shabashi, Naibu Katibu Mkuu amependeza kama dada, shangazi wa Mwanakwetu pale Mbagala!”
Hapo hapo akatamani kujua, je, Bi. Prisca amevaa mtindo gani wa mavazi?
“Hapa kiongozi wetu amevaa baibui nyeusi, kofia na mtandio. Kwa utaratibu wa uvaaji wa baibui, wanawake wa Pwani ya Tanzania wana desturi ya kuvaa baibui na kofia, baibui na mtandio, au baibui, kofia na mtandio kwa pamoja.”
Hayo yalikuwa maelezo ya Bi. Queen Simkwassa, mwanafunzi wa mafunzo kwa vitendo kazini katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, jijini Dodoma.
“Hapa picha inaonesha baibui nyeusi, mtandio mweusi na kilemba bini kofia chenye maua maua ndani ya mtandio.”
Alimalizia maelezo yake Bi. Simkwassa.
Baada ya kupata majibu hayo, Mwanakwetu moyoni alitamani kumtumia Naibu Katibu Mkuu zawadi ya kumpongeza kwa kupendeza kwake.
Hata hivyo, akawa anajiuliza: Je, zawadi hiyo itamfikiaje kiongozi huyu?
“Je, mimi Mwanakwetu wa Mbagala nitaweza kuvuka ngome zote hadi kumfikishia zawadi hiyo kiongozi huyu?”
Mwanakwetu akaamua kubakia kimya.
Lakini mwisho wa siku, akaamua kuyaandika makala haya kama njia ya kujifariji, huku akiwa na ndoto moyoni ya kumzawadia kiongozi huyo.
Bado swali likabaki: Zawadi hiyo itamfikishaje?
Katika kufuatilia mkutano huu unaohusu masuala ya rasilimaliwatu katika Mkutano wa 11 wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimaliwatu katika Sekta ya Umma Afrika (APS HRMNET), unaofanyika Zanzibar, Mwanakwetu alibaini mambo mawili muhimu.
Jambo la kwanza:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri anayehusika na masuala ya Utumishi wa Umma wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Jean-Pierre Lihau Ebua, Novemba 11, 2026, Zanzibar.
Mazungumzo hayo yalilenga kujadili fursa za kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika masuala ya usimamizi na maendeleo ya Utumishi wa Umma, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu bora za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Jambo la pili:
Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, nayo inashiriki mkutano huu, ikiwa inawakilishwa na maafisa wake wawili: Bi. Salama Said Mohammed, ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, na Bi. Victoria Alfred Mgimba, ambaye ni Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi.
Huku Novemba 13, 2026, ikiwa ni siku ya kuhitimisha mkutano huo, na pengine Naibu Katibu Mkuu, Bi. Prisca Lwangili, atakaporejea Dodoma, Mwanakwetu atatafuta wasaa wa kumkabidhi zawadi yake.
Makala haya yawe ni bashirafu ya zawadi hiyo.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka:
“BAIBUI YA NAIBU KATIBU MKUU.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)










.gif)
Post a Comment