Anyimwa uhuru wa kushangilia kisa mapenzi ya jinsia moja


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Nyota wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Felix Nmecha, ameingia kwenye mjadala baada ya aina yake ya kushangilia mabao kuhusishwa na mtandao wa kidini unaokosolewa kwa misimamo yake dhidi ya ushoga na watu wenye utambulisho tofauti wa kijinsia.

Mjadala huo ulichukuwa nafasi baada ya Nmecha kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-1 wa Dortmund dhidi ya SV Elversberg, Novemba 7, 2026. Baada ya kufunga, mchezaji huyo alionekana akiondoa taji la kufikirika kichwani na kuliweka chini, ishara inayohusishwa na kampeni ya The King's Return inayotumiwa na mtandao wa wanamichezo Wakristo unaojulikana kama Ballers in God.

Kutokana na hali hiyo, idara ya mashabiki ya Borussia Dortmund ilitoa msimamo ikieleza kuwa haipingi haki ya mchezaji kuonesha imani yake kupitia ushangiliaji wake, bali inapinga matumizi ya imani au mitandao ya kidini katika kuwatenga na kuwashusha hadhi watu wengine.

Rais wa klabu hiyo, Hans Joachim Watzke, pia alizungumza na Nmecha na kumshauri afikirie kuachana na ushangiliaji huo unayohusisha kuweka taji chini, akieleza kuwa ishara hiyo inaweza kuhusishwa na mtandao huo na kuleta mgawanyiko miongoni mwa mashabiki.


Kwa upande wake, Nmecha alieleza kuwa hakuwa na nia ya kueneza chuki, ubaguzi au kutangaza mtandao wowote, amesema kwake kitendo hicho ni ishara ya imani yake ya Kikristo na kumkabidhi Yesu Kristo heshima yote.

Hata hivyo, mjadala huo umefika pia katika timu ya taifa ya Ujerumani, ambapo kocha Jurgen Klopp alithibitisha kuwa amezungumza na Nmecha kuhusu namna ushangiliaji huo unavyotafsiriwa na watu wengine. Baada ya mazungumzo hayo, Klopp alisema wamekubaliana kuwa Nmecha hataendelea kutumia aina hiyo ya ushangiliaji anapokuwa na timu ya taifa.

Kwa mantiki hiyo, suala la Nmecha limeibua mjadala kuhusu mipaka kati ya uhuru wa mchezaji kuonesha imani yake binafsi na wajibu wa klabu za soka kuhakikisha mazingira ya michezo yanaheshimu watu wote bila ubaguzi.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments