Ukarabati wa miundombinu ya michezo uwe utamaduni hata baada ya Afcon


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Ukarabati wa viwanja nchini usisubiri Tanzania inapopata nafasi ya kuandaa mashindano makubwa, bali uwe sehemu ya utamaduni wa maendeleo ya michezo.

Baada ya Tanzania kuwa miongoni mwa wenyeji wa AFCON 2027, mchakato wa kuboresha miundombinu ya michezo umechukua nafasi kubwa, ikiwemo ukarabati wa viwanja, ujenzi wa Uwanja wa Arusha pamoja na viwanja vya mazoezi.

Hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya michezo nchini, hata hivyo, kinachopaswa kuangaliwa zaidi ni namna ya kufanya maboresho hayo yaendelee hata baada ya mashindano kumalizika.

Viwanja vinapaswa kuwa tayari kutumika muda wote na kwa michezo mbalimbali, hii itaongeza ubora wa mashindano ya ndani, kuwapa wachezaji mazingira bora ya kucheza na pia kuwavutia vijana zaidi kuupenda na kuutumia mchezo kama sehemu ya maisha yao pia itawavuta mashabiki uwanjani kutokana na ubora wake.

Kwa mantiki hiyo, ukarabati unaofanyika kuelekea AFCON 2027 unapaswa kuwa mwanzo wa utamaduni mpya wa kutunza na kuboresha viwanja, badala ya kuwa zoezi linalofanyika kila tunapopata mashindano makubwa.


Aidha, viwanja vya zamani, ikiwemo vinavyomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi, vinahitaji kupewa kipaumbele katika mpango huo, uwekezaji katika ukarabati unapaswa kwenda sambamba na utunzaji, ulinzi na matumizi sahihi ya viwanja hivyo ili visirudi katika hali ya awali baada ya muda mfupi.

Tanzania inahitaji mfumo ambao unafanya viwanja kuwa tayari wakati wote, Fursa ya kuandaa mashindano makubwa inaweza kuja wakati wowote, lakini maandalizi yake hayapaswi kuanza siku tunapotangaziwa kuwa wenyeji.

AFCON 2027 inaweza kuwa sababu ya kuongeza kasi ya maboresho, lakini isiwe mwisho wa marekebishi Kinachotakiwa ni kuifanya michezo nchini iwe na miundombinu inayotunzwa na kuboreshwa kila mwaka.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments