Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Tanzania ina viwanja vingi vya mpira wa miguu vyenye ubora na miundombinu inayowezesha michezo kuchezwa katika mazingira mazuri. Hata hivyo, linapokuja suala la viwanja vinavyotumia nyasi asilia, uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo Babati mkoani Manyara, ni miongoni mwa viwanja vinavyostahili kupewa pongezi kwa namna eneo lake la kuchezea linavyotunzwa.
Uwanja huo unatumika katika michezo ya ligi kuu , ukitumiwa na klabu ya Fountain gate kama uwanja wa nyumbani na umekuwa miongoni mwa viwanja vyenye eneo zuri la kuchezea ukiruhusu mpira kutembea bila changamoto.
Ubora wa eneo la kuchezea ni sehemu muhimu katika mchezo wa soka, Uwanja unapokuwa na nyasi zilizo katika hali nzuri, wachezaji hupata mazingira mazuri ya kuonesha uwezo wao, kucheza pasi na kutekeleza mbinu mbalimbali bila kuvuruga mpango wa uchezaji.
Tanzanite Kwaraa ni mfano mzuri katika eneo hili, kutokana na hali ya nyasi zake na namna eneo la kuchezea linavyoendelea kutunzwa linaruhusu timu kucheza kwa uhuru na Kwa mbinu bila wasiwasi, Jambo hilo linaonesha kuwa kujenga uwanja pekee hakutoshi, bali kunahitajika pia usimamizi na utunzaji wa kila siku ili kuendeleza ubora wake.
Pongezi kubwa zinapaswa kwenda kwa meneja wa uwanja huo pamoja na Halmashauri ya Mji wa Babati kwa kusimamia na kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kuwa katika hali nzuri. Vilevile, wafanyakazi wanaohusika moja kwa moja na utunzaji wa eneo la kuchezea wanastahili kutambuliwa kwa juhudi zao.
Ni muhimu juhudi hizo zikawa mfano wa kuigwa kwa wasimamizi wa viwanja vingine nchini, hususan vile vyenye nyasi asilia ambavyo baadhi yake hulalamikiwa kwa kuwa vibovu katika eneo la kuchezea kwa sababu nyasi asilia zinahitaji uangalizi wa karibu, umwagiliaji, ukataji na matunzo ya mara kwa mara ili kuendelea kuwa katika hali inayokidhi mahitaji ya mchezo.
Tanzanite Kwaraa inatoa somo kwamba ubora wa uwanja hauishii kwenye majengo, majukwaa au ukubwa wake, bali unaonekana pia katika namna eneo la kuchezea linavyohudumiwa na hapo ndipo juhudi za wasimamizi na watunzaji wa uwanja zinapopaswa kuthaminiwa.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment