Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Physical Education au elimu ya viungo na michezo, ni sehemu ya elimu inayomfundisha mwanafunzi kushiriki katika mazoezi na michezo kwa lengo la kujenga afya, uwezo wa mwili, nidhamu na ushirikiano Lakini zaidi ya hapo, somo hili linaweza kuwa njia ya kutambua na kukuza vipaji vya michezo tangu mtoto akiwa shuleni.
Michezo imeendelea kuwa sehemu ya maisha ya vijana na pia chanzo cha ajira, wapo wanaopata kipato kupitia uchezaji, ukocha, uamuzi, uandishi wa habari za michezo, usimamizi na taaluma nyingine zinazohusiana na michezo. Kupitia michezo pia, baadhi ya Watanzania wamepata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Kutokana na nafasi hiyo, Physical Education inapaswa kupewa kipaumbele katika mfumo wa elimu, kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, Somo hili linapofundishwa kwa vitendo, wanafunzi wanapata nafasi ya kuonyesha uwezo wao na vipaji vinaweza kutambuliwa mapema.
Hili pia litasaidia kuongeza wataalamu katika sekta ya michezo. Wanafunzi wanaweza kuendelea na taaluma mbalimbali kama ukocha, ualimu wa michezo, usimamizi wa michezo, mazoezi ya viungo na maeneo mengine yanayohusiana na sekta hiyo.
Pamoja na hilo, ingekuwa hatua nzuri kuwa na vyuo au taasisi maalumu zinazolenga taaluma za michezo, taasisi hizo zinaweza kutoa mafunzo ya kitaalamu na kusaidia kukuza wanamichezo pamoja na wataalamu wanaoweza kufanya kazi ndani na nje ya Tanzania.
Kwa hiyo, michezo isiishie kuwa shughuli ya baada ya masomo au burudani inapaswa ijengwe ndani ya mfumo wa elimu ili shule ziwe sehemu ya kugundua vipaji, vyuo sehemu ya kuvikuza na sekta ya michezo iwe sehemu ya kuvigeuza kuwa taaluma na ajira.
Kuwekeza katika elimu ya michezo ni kuweka msingi wa kuzalisha wanamichezo na wataalamu ambao wanaweza kujiajiri, kuajiriwa na kuiwakilisha Tanzania katika jukwaa la kimataifa.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment