Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
“Kamati iliyotangazwa ni haramu na haiwezi kufanya chochote, Kamati tutaitangaza na anayetaka fomu achukue agombee. Sio lazima Mangungu niwe mwenyekiti, ila nataka kipindi hiki ninachoongoza basi utaratibu ufuatwe wala sio kushambuliana,” amesema Murtaza Mangungu, Mwenyekiti wa Simba SC.
Anachokifanya Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu, ni kuibua mjadala ndani ya klabu hiyo wakati ambao timu ipo kwenye kiwango bora kwenye ligi na inaendelea na maandalizi kuelekea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mangungu amezungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo kusema kuwa kamati ya uchaguzi iliyotangazwa ni haramu.
Swali ni je, kamati hiyo ilipotangazwa, Mangungu alikuwa wapi? Ikumbukwe kuwa Mangungu ni Mwenyekiti wa Simba SC na pia Makamu Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi, Hivyo, kauli yake kuhusu uhalali wa kamati hiyo inazua maswali kuhusu nafasi yake katika mchakato huo.
Klabu ya Simba inaelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari 2027, huku muda wa uongozi wa sasa ukikaribia tamati Katika hali hii, kauli za Mangungu zinaweza kuongeza mjadala miongoni mwa wanachama kuhusu uchaguzi huo na uwezekano wa yeye kuwania muhula mwingine . Hata hivyo, hilo linahitaji kuthibitishwa kupitia kauli au hatua zake rasmi.
Kwa ujumla, si ukomavu kwa kiuongozi kuibua masuala yanayoweza kuathiri umoja wa klabu bila kuhakikisha kuwa tofauti zilizopo zinajadiliwa na kutatuliwa kwa kufuata taratibu za ndani. Ingekuwa bora zaidi masuala hayo yakajadiliwa katika vikao vya klabu kabla ya kuzungumzwa hadharani, ili kuepusha sintofahamu wakati Simba ikiendelea na kampeni zake za Ligi Kuu Tanzania Bara na maandalizi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.

Post a Comment