Mussa wa Simba mbioni kufika nchi ya asali na maziwa

 Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kuna wakati wana wa Israeli walipitia nyakati ngumu wakielekea nchi ya ahadi, nchi ya maziwa na asali waliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu. Katikati ya safari hiyo, walikuwa na kiongozi wao, Mussa, aliyewatia moyo na kuwaongoza kukabiliana na magumu waliyopitia kwa msaada wa Mwenyezi Mungu.



Katika soka la Tanzania, klabu ya Simba ni mfano wa hadithi hiyo kupitia msemaji wake, Ahmed Ally, aliyejitwika jukumu la kuwavusha Wanasimba kutoka kwenye nyakati ngumu za kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu mitano mfululizo, huku hali hiyo ikichagizwa na vipigo sita mfululizo kutoka kwa mtani wao ama hakika ilikuwa safari ngumu yenye majonzi na mateso kwa mashabiki wa klabu hiyo.



Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa ligi ilikuwa msimu wa 2020/21, tangu wakati huo, klabu hiyo imeendelea kutafuta namna ya kurejesha taji hilo lililokuwa sehemu ya mafanikio yao.

Kupitia ucheshi wake, Ahmed amekuwa akiwafurahisha Wanasimba katika nyakati ngumu kama sehemu ya kuwatia moyo, Katika kipindi cha mgawanyiko, amekuwa akisimama kuhamasisha umoja, huku hekima na busara zake za kuelewa wakati gani azungumze nini zikichangia kuimarisha mshikamano miongoni mwa mashabiki wa Simba.



Akiwa kama Mussa wa Msimbazi, Ahmed sasa anaendelea kutumia hamasa zake katika safari ya kuielekeza Simba kwenye nchi ya ahadi, yaani ubingwa walioukosa kwa misimu mitano mfululizo. Hili linakuja wakati timu hiyo ikiwa na kiwango kizuri katika msimu huu wa 2026/27, hali inayowapa Wanasimba matumaini ya kurejea kwenye ubingwa wa ligi kuu na kufanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika.

Hakika, katika mafanikio ya Simba, jina la Ahmed Ally linastahili kutajwa kwa nafasi yake ya kuhamasisha mashabiki na kuimarisha mshikamano wao, hata hivyo, si yeye pekee aliyeibeba klabu hiyo katika safari hii, kwani kuna juhudi za viongozi, benchi la ufundi na wachezaji. Lakini kwa nafasi yake kama msemaji, Ahmed amekuwa na mchango wake katika kuifanya safari ya Simba iendelee kuwa na matumaini.


0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.

0/Post a Comment/Comments