Msanii aliyeshuka jukwaani wakati watazamaji wakiwa wamenogewa na burudani


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Machozi mengi yenye hisia kali mara nyingi humwagika pale mtu anapokuwa ameupa mgongo ulimwengu Lakini kwa Lionel Messi imekuwa tofauti. Akiwa bado pamoja na ulimwengu, ameshuhudia machozi yakimwagika, akililiwa na kuonyeshwa upendo ambao mara nyingi watu huupata baada ya kuaga dunia au wanapokuwa kwenye taabu.

Mchezo wa kirafiki kati ya Argentina dhidi ya Benin uliopigwa dimba la Estadio Monumental uliimaliza safari ya Messi huku akiisindikiza kwa bao Moja na pasi mbili za mabao na kuhitimisha kalamu ya 3-0 waliyoipata Argentina kwenye usiku wa historia 


Maneno, heshima na historia nzuri vimesemwa akiwa anasikia, ameuona upendo ambao wengi hupewa wakiwa hawapo tena, Kwa Messi, imekuwa tofauti na jambo hilo limegusa nafsi za wafu na walioko hai.

Nyota huyo aliwahi kuitwa “A man from another planet”, kutokana na mambo aliyowahi kuufanyia mpira akiwa dimbani, Uwezo wake wa kuchezea mpira, kufunga na kutengeneza nafasi ulimpa nafasi ya kipekee miongoni mwa mamilioni ya wachezaji duniani.

Lakini ubora wake haupimwi kwa maneno pekee , Messi ameshinda Ballon d'Or nane, Kombe la Dunia moja, Copa America mbili, Finalissima moja, medali ya dhahabu ya Olimpiki moja na Kombe la Dunia la U-20 moja.


Katika timu ya taifa ya Argentina alianza mwaka 2005, kabla ya kufikia mwisho wa safari yake ya kimataifa mwaka 2026.

Hakika hii ni “last dance.” Messi amekuwa kama msanii aliyeshuka jukwaani wakati watazamaji bado wamenogewa na burudani hii ni kutokana na Ufanisi wake kwenye jukwaa la soka ambao umefanya kila mmoja atamani kuendelea kumtazama, lakini wakati wa kuaga umefika.

Miaka zaidi ya 20 ya kuiona Argentina ikiwa na Messi imefika mwisho, Kile kinachobaki ni kumbukumbu za magoli, mataji, pasi, dribbling na nyakati ambazo zilifanya mamilioni ya watu kukaa mbele ya televisheni wakisubiri kuona kitu kutoka kwake.


Sasa maisha mapya yanaanza, Messi hatacheza tena kwenye timu ya taifa ya Argentina, lakini ataendelea na safari yake ya soka akiwa na Inter Miami, hadi siku atakapoamua kuaga rasmi soka.

Na pengine uzuri wa hadithi yake haupo tu katika namna alivyoondoka, bali katika ukweli kwamba ameweza kushuka jukwaani wakati bado watu walikuwa wanamtaka aendelee kucheza.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com






0/Post a Comment/Comments