Mataifa yamesadiki jina lake, Tanzania impe heshima yake


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports

Kuna wachezaji wanaocheza soka kwa ajili ya mafanikio ya klabu zao, lakini wapo wanaovuka mipaka ya nchi zao na kuwa sehemu ya utambulisho wa taifa. Kwa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ni miongoni mwa wachezaji waliofikia hatua hiyo kupitia safari yake ya soka ndani na nje ya nchi.

Baada ya kutumikia Taifa Stars kwa kipindi kirefu, Samatta ametangaza kustaafu kuichezea timu hiyo, Uamuzi huo unafunga ukurasa muhimu katika historia yake ya kimataifa, lakini pia unaibua swali kuhusu namna taifa linavyopaswa kumuaga mmoja wa wachezaji walioitambulisha nchi katika majukwaa makubwa ya soka duniani.

Safari ya Samatta ilianzia katika soka la Tanzania, akipitia African Lyon na Simba SC kabla ya kujiunga na TP Mazembe ya Congo DRC 2011na huko ndiko alikopata mafanikio yaliyomfungulia milango ya soka la kimataifa.

Akiwa TP Mazembe, Samatta alisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 huku akimaliza mashindano hayo akiwa mfungaji bora kwa mabao saba, kisha akashinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika anayecheza ndani ya Afrika ya CAF.

Mafanikio hayo yalikuwa mwanzo wa safari yake katika soka. Mnamo Januari 2016, alijiunga na KRC Genk ya Ubelgiji na kuendelea kutengeneza jina katika soka la Ulaya.

Msimu wa 2018/19 ulikuwa miongoni mwa misimu bora kwa nyota huyo kwani aliisaidia Genk kutwaa ubingwa wa ligi ya Ubelgiji na kufunga mabao 20 ya ligi, akimaliza akiwa mfungaji bora wa mashindano hayo.


Januari 2020, alijiunga na Aston Villa na kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England lakini baadaye aliendelea na safari yake na fenerbahche ya Uturuki, Royal Antwerp ya Ubelgiji na PAOK ya Ugiriki, kabla ya kujiunga na Le Havre ya Ufaransa mwaka 2025.

Kucheza katika Premier League na Ligue 1, miongoni mwa ligi tano kubwa za Ulaya, ni sehemu ya historia inayoweka wazi kiwango alichofikia Samatta,Safari yake imeonyesha kuwa ni mchezaji mwenye juhudi na kujituma na ni mfano bora wa kuigwa na vijana kwenye kiwanda Cha soka nchini.

Mchango wake hauishii katika klabu alizochezea, Kwa miaka mingi Samatta aliitumikia Taifa Stars, akiwa nahodha na mmoja wa wachezaji waliobeba matumaini ya Watanzania katika mashindano ya kimataifa.


Alikuwa sehemu ya kikosi kilichoiwezesha Tanzania kufuzu AFCON 2019 nchini Misri, baada ya kusubiri kwa miaka 39 tangu ushiriki wake wa mwisho mwaka 1980, Pia aliendelea kuiwakilisha nchi katika safari za AFCON zilizofuata, akichangia katika historia ya soka la taifa.

Sasa, baada ya kutangaza kustaafu kuichezea Taifa Stars, Tanzania inapaswa kutafakari hatua inayofuata, huu si wakati wa kuzungumzia siku ya kumuenzi Samatta kila mwaka, bali ni wakati wa kuandaa siku maalumu ya kumuaga kwa heshima mchezaji huyo baada ya kuitumikia nchi kwa kipindi kirefu.


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya michezo na wadau wengine, wanapaswa kuandaa hafla rasmi ya kumuaga Samatta hafla hiyo inaweza kuambatana na mchezo maalumu wa heshima utakaomshirikisha yeye, wachezaji wenzake wa zamani, Taifa Stars na wadau wa soka nchini.

Hiyo itakuwa nafasi ya Watanzania kumshukuru kwa mchango wake, kumpongeza kwa mafanikio aliyoyapata na kumpa heshima anayostahili baada ya miaka ya kulitumikia taifa. Pia itakuwa fursa ya kurekodi rasmi historia yake ili vizazi vijavyo vijue safari ya mchezaji aliyeanzia nyumbani na kufika katika majukwaa makubwa ya soka duniani.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments