Klabu zilizotawala ligi tano Ulaya kwa misimu kumi



Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Katika soka la Ulaya, kutwaa ubingwa ni mafanikio yanayohitaji maandalizi, usajili wenye tija na mwendelezo wa matokeo, hata hivyo, kutawala ligi kwa kipindi cha miaka mingi ni kipimo kinachoonyesha uwezo wa klabu kujenga timu inayoweza kushindana licha ya mabadiliko ya wachezaji na makocha.

Katika misimu kumi kuanzia 2016/17 hadi 2025/26, ligi tano kubwa za Ulaya zimekuwa na klabu zilizoweka alama kwa idadi ya mataji na kuwa klabu tawala katika Ligi zao.

Bundesliga ya Ujerumani inaongozwa na Bayern Munich, iliyotwaa mataji tisa kati ya kumi. Mafanikio hayo yanaonyesha uwezo wa klabu hiyo kuishi kwenye ushindani kwa muda mrefu, huku klabu ya Bayer Leverkusen ikivunja mfululizo wa mataji ya Bayern kwa kutwaa ubingwa wa msimu wa 2023/24, ikionyesha kuwa hata timu iliyotawala kwa muda mrefu inaweza kupokonywa nafasi yake.

Nchini Ufaransa, klabu ya PSG imetwaa mataji nane ya Ligue 1 katika kipindi hicho, Uwezo wa klabu hiyo kuimarisha kikosi na kuwa na wachezaji wenye viwango vya juu umeifanya kuwa na nguvu kubwa katika soka la ndani huku Lille na Monaco nazo zimefanikiwa kuvunja utawala huo kwa kutwaa taji moja kila moja katika kipindi hicho.

Katika Premier League ya England, Manchester City inaongoza kwa mataji sita, huku Liverpool ikiwa na mawili, Chelsea na Arsenal zimechukua taji moja kila moja. Mafanikio ya City yanaonyesha umuhimu wa kuwa na mfumo wa uchezaji unaoeleweka, kikosi chenye uzoefu wa kukaa kwa pamoja na uwezo wa kusimamia kiwango katika michezo mingi ya ligi.

LaLiga ya Hispania imekuwa na ushindani mkubwa kati ya Barcelona na Real Madrid lakini Barcelona inaongoza kwa mataji matano, ikifuatiwa na Real Madrid yenye manne, huku Atletico Madrid ikiwa na taji moja,tofauti hiyo ndogo inaonyesha kuwa licha ya vipindi vya utawala wa klabu moja, ushindani kati ya wapinzani wakubwa unaweza kubadilisha mwelekeo wa mbio za ubingwa.

Kwa upande wa Serie A ya Italia, Juventus inaongoza kwa mataji manne, yote yakipatikana katika misimu minne mfululizo kuanzia 2016/17 hadi 2019/20. Inter Milan imefuatia kwa mataji matatu, Napoli ikiwa na mawili na AC Milan ikiwa na taji moja, mabadiliko hayo yanaonyesha namna ushindani wa Italia ulivyoenea zaidi baada ya kipindi cha Juventus kutawala.

Kwa kujumlisha mafanikio hayo, Bundesliga ina klabu iliyotwaa mataji mengi zaidi katika ligi moja ndani ya kipindi hiki kupitia Bayern Munich yenye mataji tisa. PSG inafuatia kwa mataji nane ya Ligue 1, Manchester City ikiwa na sita ya Premier League, Barcelona ikiwa na matano ya LaLiga na Juventus ikiwa na manne ya Serie A.


Kwa ujumla, misimu hii kumi inaonyesha kuwa kutawala ligi kunahitaji zaidi mwendelezo na uimara kwenye benchi la Ufundi, huku kuwa na wachezaji kwenye kikosi wale wale kwa muda mrefu kukitengeza maelewano kiuchezaji na ndio inakuwa mwanzo wa mafanikio.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments