Kilichopo nyuma ya pazia urejeo wa Doumbia kambani


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kwa mshambuliaji, kufunga mabao ni sehemu muhimu ya majukumu yake, lakini nyakati nyingine ukimya wa muda mrefu mbele ya lango unaweza kuathiri kujiamini na kufanya kila nafasi anayoipata ionekane kuwa na presha kubwa.

Hali hiyo ndiyo iliyokuwa ikimkabili mshambuliaji wa Simba SC raia wa Mali Ibrahim Doumbia, ambaye alitoka kwenye michezo 14 ya kimashindano bila kufunga bao tangu ajiunge na mnyama, hata hivyo, baada ya kipindi hicho kigumu, nyota huyo ameanza upya kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa 6-1 wa Simba dhidi ya 15 de Agosto kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini nyuma ya kurejea kwake kwenye orodha ya wafungaji, jina la Denzel Trainer haliwezi kuachwa pembeni.



Trainer huyo, ambaye amekuwa akifanya kazi na wachezaji mbalimbali wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika eneo la utimamu wa mwili, alitoa waraka kupitia mtandao wa kijamii akiwahimiza wachezaji kutokata tamaa wanapopitia nyakati ngumu, akisisitiza kuwa kila mchezo ni nafasi ya kujifunza na kuimarika.

Ujumbe huo unaendana na hali aliyokuwa akiipitia Doumbia, ambaye alihitaji kurejesha makali yake mbele ya lango na kujiamini baada ya kukosa mabao katika michezo 14 ya kimashindano.

Kupitia programu ya mazoezi aliyomfanyia mshambuliaji huyo, Trainer alichangia katika maandalizi yake ya kurejea kwenye kiwango bora, Kisha Doumbia akajibu kwa vitendo uwanjani, akifunga mabao mawili katika ushindi huo wa Simba, matokeo yaliyomfungulia ukurasa mpya katika safari yake ya msimu huu.

Hata hivyo, kurejea kwa mshambuliaji katika kiwango bora hakutegemei jambo moja pekee. Utimamu wa mwili, maandalizi ya kiakili, ubora wa mazoezi na matumizi bora ya nafasi ni sehemu ya mambo yanayoweza kuongeza uwezo wa mchezaji kufunga. Kwa Doumbia, mabao hayo mawili ni mwanzo wa matumaini mapya baada ya kipindi kirefu cha kusubiri.

Denzel Trainer si mgeni katika kufanya kazi na wachezaji wa soka, hasa katika kuwaandaa kimwili na kuwasaidia kurejea kwenye hali nzuri, miongoni mwa wachezaji ambao wamehusishwa na kazi zake ni Pacome Zouzoua, Max Nzengeli, Kibabage ,Dickson Job na Mwamnyeto, pamoja na wengine wanaoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ushirikiano wa wataalamu wa utimamu wa mwili na wachezaji ni sehemu ya maandalizi ya kisasa ya soka, ambako mafanikio hayajengwi siku ya mchezo pekee, bali pia katika mazoezi, nidhamu na maandalizi yanayofanyika nje ya uwanja.



Kwa Simba, kurejea kwa Doumbia katika orodha ya wafungaji ni habari njema, hasa ikizingatiwa umuhimu wa kuwa na washambuliaji wanaoweza kutumia nafasi wanazopata katika mashindano ya ndani na kimataifa. Mabao yake mawili dhidi ya 15 de Agosto yanaweza kuwa chachu ya kuendelea kujenga kujiamini na kutafuta mabao zaidi katika michezo inayofuata.

Kwa Doumbia, ukame wa mabao wa michezo 14 sasa umevunjwa, Kwa Denzel Trainer, mchango wake katika maandalizi ya mshambuliaji huyo umeingia kwenye mjadala unaozunguka kurejea kwa nyota huyo. 

Safari ya Doumbia ya kurejea kwenye makali imeanza, Sasa mtihani wake ni kuendeleza kiwango hicho na kuthibitisha kuwa mabao mawili dhidi ya 15 de Agosto ni mwanzo wa ukurasa mpya wa ufungaji.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments