Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
“Kwenye kila mafanikio ya mtu kuna mtu nyuma yake.” Kauli hii imevaa uhalisia kuanzia kwenye maisha ya kawaida ya kila siku na kugusa uwanda wa soka kwa namna yake.
Klabu ya Simba SC ni miongoni mwa klabu kubwa nchini Tanzania kutokana na ubora wake, ikiwemo kutwaa mataji, hata hivyo, katika mafanikio ya Wekundu wa Msimbazi, kuna jambo ambalo wengi hawajalipa uzito unaostahili, mchango wa Azam FC katika kukisuka kikosi cha Simba.
Kwa misimu minne mfululizo ambayo Simba ilitawala Ligi Kuu Tanzania Bara, kuanzia 2017/18 hadi 2020/21, klabu hiyo ilisajili wachezaji kutoka Azam FC ambao waliongeza nguvu katika kikosi na kuchangia mafanikio ya kutwaa ubingwa wa ligi mara nne mfululizo.
Majina kama Aishi Manula, John Bocco, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe ni miongoni mwa wachezaji waliotoka Azam na kujiunga na Simba mwaka 2017.
Manula alikuwa nguzo katika lango la Simba, huku kiwango chake kikimfanya kutambulika kwa jina la "Tanzania One". Kwa upande mwingine, John Bocco alichangia safu ya ushambuliaji kwa kufumania nyavu na kusaidia timu kupata matokeo.
Erasto Nyoni aliongeza Ufanisi katika dimba huku uzoefu na uwezo ukiibeba timu mabegani kwa nyakati tofauti tofauti. Kwa upande wa Shomari Kapombe ametoa mchango wake katika ulinzi wa pembeni Kwa kiwango ambacho hakijawahi kuchukua, Kwa pamoja, wachezaji hao walikuwa sehemu ya kikosi kilichosaidia Simba kutwaa mataji ya ligi katika kipindi hicho.
Sasa, miaka kadhaa baadaye, Simba imechukua hatua nyingine kwa kumsajili Nathaniel Chilambo kutoka Azam FC.
Akiwa Azam, Chilambo alikumbana na changamoto ya majeraha yaliyomzuia kupata nafasi ya kudumu katika kikosi, hata hivyo, Simba imeona fursa ya kumsajili na kumpa nafasi ya kuendeleza uwezo wake Msimbazi.
Nathaniel si suala la jina pekee, bali ni namna anavyoweza kutumika katika maeneo tofauti ya uwanja akiwa beki wa pembeni, anaweza pia kusaidia katikati ya dimba na kuongeza machaguo ya kiufundi kwa benchi la ufundi.
Kwa upande wa Feisal Salum, maarufu kama Fei Toto, bado hakuna uhakika wa kujiunga na Simba, hata hivyo, uwezekano wa mchezaji huyo kutoka Azam na kuongeza nguvu Msimbazi unaweza kujadiliwa iwapo kutakuwa na mazungumzo na makubaliano kati ya pende mbili.
Kwa kuangalia historia hii, Azam FC imekuwa chanzo cha wachezaji waliochangia katika kikosi cha Simba, kuanzia waliotwaa mataji manne ya ligi mfululizo hadi usajili wa hivi karibuni.
Hivyo, kauli kwamba “kwenye kila mafanikio ya mtu kuna mtu nyuma yake” inaweza kutumika kueleza uhusiano huu wa kisoka, Simba imekuwa ikipata huduma za wachezaji waliotoka Azam, na kwa namna hiyo, Azam imekuwa sehemu ya hadithi ya mafanikio ya Wekundu wa Msimbazi.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment