Atletico ya Diego Simeone Yafungwa Hat-trick nne na Mchezaji Mmoja

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Makocha na wachezaji wengi wamekutana na wakati mgumu walipokabiliana na Cristiano Ronaldo katika safari yake ya soka, lakini Diego Simeone kocha wa Atletico Madrid ana rekodi inayomfanya amkumbuke mshambuliaji huyo katika historia ya michezo yao.

Tangu Simeone aanze kuifundisha Atletico Madrid mwaka 2011, Ronaldo amekuwa miongoni mwa wachezaji waliompa wakati mgumu zaidi, akifunga hat-trick nne dhidi ya timu hiyo katika vipindi tofauti na akiwa ndiye mchezaji pekee aliyefanya hivyo wakati wa Simeone.

Hat-trick ya kwanza aliifunga Aprili 11, 2012, wakati Real Madrid ikiibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Atletico Madrid katika mchezo wa La Liga.


Novemba 19, 2016, Ronaldo alirudia kufanya hivyo, akiifungia Real Madrid mabao yote matatu katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Atletico Madrid.

Mei 2, 2017, aliongeza hat-trick nyingine katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya UEFA Champions League, Real Madrid ilipoichapa Atletico Madrid mabao 3-0.

Miaka miwili baadaye, Machi 12, 2019, akiwa Juventus, Ronaldo alifunga hat-trick yake ya nne dhidi ya Atletico Madrid katika ushindi wa 3-0 wa mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora ya UEFA Champions League.


Rekodi hiyo inaweka wazi namna Ronaldo alivyokuwa mwiba kwa Atletico Madrid katika kipindi ambacho Simeone amekuwa akiiongoza timu hiyo, Katika kila moja ya matukio hayo manne, Ronaldo alifunga mabao matatu katika mchezo mmoja, akionyesha uwezo wake wa kuamua matokeo katika michezo yenye ushindani mkubwa.

Sambamba na rekodi hiyo pia Simeone alishawahi kukiri kuwa asingekuwa Ronaldo basi huenda angekuwa na taji la Uefa champions league, na katika safari yake kama kocha , mchezaji huyo amekuwa mwiba wa mateso kwa vipindi walivyo kutana.

0767815473,

lugembetimothy01@gmail.com.

0/Post a Comment/Comments