Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports
Kufuzu Kombe la Dunia kulionekana kama mwanzo wa safari mpya kwa timu ya taifa ya Cape Verde, lakini kuelekea Afrika Mashariki mambo yameanza kuwa tofauti.
Cape Verde iliandika historia katika Kombe la Dunia 2026 baada ya kufuzu hatua ya 32 bora, ambapo ilikutana na Argentina na kuondolewa baada ya kufungwa mabao 3-2, hakika haikuwa kinyonge walionyesha ukomavu wa hali ya juu licha ya uchanga wao kwenye michuano hiyo
Mafanikio hayo yaliifanya Cape Verde kuingia kwenye orodha ya timu zilizokuwa zikisubiriwa kwa hamu kuonyesha makucha kwenye mashindano ya Afrika, huku ikishika nafasi ya 53 katika viwango vya FIFA.
Hata hivyo, baada ya Kombe la Dunia, timu hiyo imeanza kampeni za kufuzu AFCON 2027 kwa matokeo ambayo hayakutarajiwa.
Cape Verde imepoteza michezo yake miwili ya kwanza katika Kundi K, ikianza kwa kufungwa 3-1 na Mali kabla ya Rwanda kuiongezea maumivu kwa ushindi wa 2-1.
Matokeo hayo yameiacha Cape Verde mkiani mwa kundi ikiwa haina alama, wakati bado ikiwa na michezo minne ya kujaribu kubadilisha hali hiyo na kuwania nafasi ya kufuzu AFCON 2027, ambayo itafanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
Hapa ndipo safari yao inapokuwa na mtihani mwingine, baada ya kizazi cha sasa kufikisha timu kwenye hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia, mwenendo wa sasa unaibua swali kama bado kina uwezo wa kuendelea kuibeba Cape Verde au muda umefika wa kuanza kuandaa kizazi kingine.
Kwa Cape Verde, Kombe la Dunia lilikuwa sehemu ya kuandika historia. Sasa, kuelekea Afcon 2027 Afrika Mashariki wanatakiwa kuhakikisha historia hiyo haiishii kwenye kumbukumbu pekee.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.



Post a Comment