Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Zamani, timu kutoka Tanzania ziliposhiriki michuano ya kimataifa, wachezaji wake walitumia michezo hiyo kama jukwaa la kuonyesha viwango ili kupata nafasi ya kuonekana na kusajiliwa na vilabu vya nje.
Simba na Yanga zilipokuwa zikikabiliana na timu kutoka mataifa mbalimbali, wachezaji walikuwa na ndoto ya kutumia michuano hiyo kama daraja la kwenda kwenye ligi nyingine, hasa katika ukanda wa Kaskazini na Magharibi mwa Afrika, pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Lakini sasa upepo umeanza kubadilika ambapo timu za Tanzania zinapokutana na wapinzani kutoka nje, si jambo la kushangaza kuona wachezaji wa timu hizo wakitamani kupata nafasi ya kucheza nchini Tanzania. Badala ya Tanzania kuwa soko la wachezaji wanaotafuta kwenda nje, sasa ligi hiyo imeanza kuwa sehemu ambayo wachezaji kutoka mataifa mengine wanaiona kama fursa ya kujenga au kuendeleza taaluma zao.
Hii si kwa bahati , Ligi Kuu Tanzania Bara imeendelea kujenga mazingira yanayovutia wachezaji kutoka mataifa mbalimbali huku Simba, Yanga na vilabu vingine vimekuwa na wachezaji kutoka nje, na ushindani wa ligi ukiongezeka na michezo ya kimataifa ikiendelea kuitangaza Tanzania.
Moja ya mambo yanayochangia mabadiliko hayo ni miundombinu inayozidi kuboreshwa. Viwanja, vituo vya mazoezi na mazingira ya michezo inaendelea kutoa msingi unaohitajika kwa ligi yenye ushindani.
Pamoja na hilo, suala la stahiki za wachezaji limekuwa sehemu nyingine ya mvuto, Malipo yanapokuwa na uhakika, mchezaji anaona thamani ya kuichezea ligi na anaweza kupanga maisha yake akiwa ndani ya ushindani huo.
Hata kama changamoto bado zipo, tofauti na miaka iliyopita, malalamiko ya kutolipwa kwa wachezaji hayajawa sehemu kubwa ya simulizi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pia kuna suala la matangazo ya Moja kwa moja Kupitia Azam TV, michezo ya ligi imefika kwa watazamaji ndani na nje ya Tanzania. Hii inamaanisha mchezaji wa nchi nyingine anaweza kuiona ligi bila hata kufika Tanzania, anapowaona wachezaji wenzake wakicheza, anaona vilabu, viwanja, mashabiki na mazingira ya ligi, jambo linaloweza kumfanya aanze kuifikiria Tanzania kama sehemu ya kucheza.
Hapo ndipo thamani ya ligi inapoongezeka,Tanzania haipaswi kuishia kufurahia kuwa soko linalowavutia wachezaji wa nje hatua inayofuata inapaswa kujiuliza ni nini kifanyike ili ligi ipande zaidi katika ushindani wa Afrika.
Kama tayari kuna msingi wa kuvutia wachezaji, basi miundombinu inapaswa kuendelea kuboreshwa, Stahiki za wachezaji zinapaswa kulindwa zaidi, huku vilabu vikiwekewa viwango vinavyolazimisha uwekezaji katika mazingira ya soka.
Pia ni wakati wa kuwa na mpango wa aina ya wachezaji wanaopaswa kuja kucheza Tanzania. Ikiwa ligi inalenga kupanda kutoka nafasi yake ya sasa na kuelekea kuwa miongoni mwa ligi tatu bora Afrika, basi usajili wa wachezaji nao unapaswa kuwa sehemu ya mkakati huo.
Tanzania imeanza kubadilisha taswira yake, Zamani mchezaji aliiona Tanzania kama sehemu ya kupita akitafuta soko kubwa zaidi. Sasa wapo wanaoiona Tanzania yenyewe kama soko na fursa.
Huo ni ujumbe kwamba soka la Tanzania limeanza kutambulika zaidi, Kinachobaki ni kuhakikisha upepo huo hautapita, bali unatumiwa kujenga ligi yenye ubora, ushindani na hadhi inayoweza kuifanya Tanzania kuwa moja ya vituo vikuu vya soka barani Afrika.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.

Post a Comment