Shujaa wa Yanga kupewa heshima Septemba 12


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Katika soka, wakati mwingine mchezo hauishii kwenye dakika 90 pekee Kuna nyakati ambazo uwanja huwa sehemu ya kumtambua mchezaji kwa mchango wake, kumtia moyo na kumfanya ajione kuwa sehemu ya timu anayoichezea.

Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa Yanga katika mchezo wa marudiano dhidi ya Gaborone United utakao pigwa Septemba 12, 2026 katika dimba la Azam complex ambapo klabu hiyo imechagua mchezo huo kutambua mchango wa mshambuliaji wake Selemani Mwalimu.

Mwalimu anaingia kwenye mchezo huo akiwa na kumbukumbu ya mchezo wa kwanza nchini Botswana, baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika za mwisho na kuisaidia Yanga kupata sare ya 1-1. Sasa, mchezo wa marudiano utakuwa nafasi nyingine kwake kukutana na mashabiki, safari hii wakiwa wameandaa namna ya kumuonyesha kuwa mchango wake umeonekana.

Mashabiki wa Yanga wamehamasishwa kujitokeza wakiwa na ndevu zilizopakwa rangi, kama ishara ya kumuunga mkono Mwalimu ambaye pia amekuwa akionekana na muonekano huo, hatua hiyo imepewa jina la “Mwalimu Day” au “Sele Day.”


Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kufanya jambo kama hili. Awali, mashabiki walifanya hivyo kwa Pacome, ambapo mashabiki na baadhi ya wachezaji walijitokeza wakiwa wamepaka rangi kwenye nywele zao kama sehemu ya kumuunga mkono mchezaji huyo na wachezaji wengine waliowahi kufanyiwa hivyo ni pamoja na Dickson Job, Mwamnyeto na Aziz ki.

Kwa Mwalimu, safari hii ni ndevu ndizo zitakazotumika kama alama ya heshima. Lakini nyuma ya jambo hilo kuna ujumbe mkubwa zaidi, kumfanya mchezaji ajione kuwa ni sehemu ya familia ya wananchi.

Mchezaji anapohisi kuwa mashabiki na timu wanatambua mchango wake, jambo hilo linaweza kuongeza ari ya kuendelea kuipambania timu. Hivyo, kile kinachofanywa na Yanga si igizo, bali ni njia ya kujenga uhusiano kati ya mchezaji na mashabiki, huku kikimpa sababu nyingine ya kuongeza juhudi uwanjani.

Sasa, baada ya kuanza kazi Botswana kwa bao la kusawazisha, Mwalimu anatarajiwa kuendeleza kazi hiyo mbele ya mashabiki wa Yanga katika mchezo wa marudiano.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments