Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Kwa miaka kadhaa, vilabu kutoka Tanzania vimekuwa vikijaribu kuvuka mipaka ya ndani na kufanya vizuri katika mashindano ya klabu barani Afrika lakini Safari hiyo imekuwa na matokeo tofauti, huku baadhi ya timu zikifika hatua za juu lakini zikishindwa kuchukua taji.
Simba na Yanga ni miongoni mwa klabu zilizowahi kufika hatua ya fainali ya mashindano ya CAF bila kufanikiwa kubeba vikombe hivyo, Matokeo hayo yameendelea kuwa sehemu ya historia ya safari ya Tanzania katika kutafuta mafanikio ya soka ngazi ya vilabu Afrika.
Hata hivyo, wakati umefika kwa vilabu vya Tanzania kubadili simulizi hiyo badala ya kuridhika na kufika hatua za mwisho, lengo sasa linapaswa kuwa kushinda na kuleta mataji nchini.
Mashindano ya klabu barani Afrika yanapoanza Septemba 5, 2026, vilabu vya Tanzania Bara na Zanzibar vinaingia kwenye safari nyingine ya kuwakilisha nchi, Kila timu itakuwa na nafasi ya kuonyesha uwezo wake, huku matokeo yao yakibeba sehemu ya heshima ya soka la Tanzania.
Kwa upande mwingine, mafanikio ya timu moja yanaweza kuongeza nafasi ya Tanzania kutambulika zaidi katika soka la Afrika. Ushindani unaweza kuwa sehemu ya kuendeleza kiwango cha ligi za ndani na kuwapa wachezaji nafasi ya kuonekana katika mazingira ya kimataifa.
Safari hii, jambo la msingi si timu moja pekee bali vilabu vyote vinavyowakilisha Tanzania vinahitaji kuingia kwenye mashindano hayo vikiwa na lengo moja kupiga hatua kila wanapocheza na hatimaye kuchukua ubingwa.
Tanzania imewahi kuwa karibu na mataji ya Afrika, lakini ukaribu huo haujatosha. Kinachohitajika sasa ni hatua ya mwisho ya kugeuza nafasi hizo kuwa vikombe.
Septemba 5 iwe mwanzo wa safari mpya, Safari ambayo vilabu vya Tanzania Bara na visiwani vitaingia kwa lengo la kuandika ukurasa mwingine katika historia ya soka la nchi na kuonyesha kuwa Tanzania inaweza kushindana kwa ajili ya ubingwa wa Afrika, si kushiriki pekee.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment