Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Tanzania Bara ina vipaji vingi vya soka ambavyo bado havijapata nafasi ya kuonekana katika kiwango cha ushindani wa juu, baadhi yao huendelea kucheza katika viwanja vya mitaani huku ndoto zao za kufika kwenye ligi za ushindani zikiishia njiani.
Hali hiyo inachangiwa na mambo mbalimbali, ikiwemo kutokuwepo kwa mifumo imara ya kuibua na kuendeleza vipaji katika baadhi ya maeneo. Kwa mchezaji kutoka mikoa yenye fursa chache, safari ya kufika kwenye vituo vikubwa vya soka kama Dar es Salaam au Morogoro inaweza kuwa hatua muhimu, lakini si kila mwenye kipaji ana uwezo wa kuifikia.
Kwa upande mwingine, maskauti wanaotafuta wachezaji wana nafasi ya kuangalia zaidi ndani ya Tanzania badala ya kutegemea safari za nje ya nchi pekee, viwanja vya mitaani vinaweza kuwa sehemu ya utafutaji wa vipaji, kwa kuwa huko kuna wachezaji ambao hawajawahi kupata nafasi ya kuonekana kwenye mifumo rasmi ya soka ila wanavipaji kiwango Cha ligi kuu.
Mfano unaoonekana ni mashindano ya Ndondo Cup yanayofanyika Dar es Salaam chini ya Clouds Media na washirika wengine, Mashindano hayo yamekuwa yakitoa nafasi kwa wachezaji wa mitaani kuonyesha uwezo wao mbele ya mashabiki na Wadau mbali mbali wa soka.
Baadhi ya wachezaji wanaoshiriki mashindano ya aina hiyo wana uwezo wa kucheza katika ngazi za juu, lakini hawajapata nafasi ya kuingia kwenye ligi hizo kutokana na kuto onekana kwa kazi wanayo ifanya. Hivyo, mashindano ya mitaani yanaweza kuwa daraja kati ya kipaji kilichopo kwenye jamii na soka la ushindani.
Kwa mantiki hiyo, kila mkoa unaweza kuangalia namna ya kuwa na mashindano makubwa ya ndondo yenye mfumo unaoweza kuwafanya wachezaji kuonekana na kupaisha vipaji vyao mbali zaidi, Wadhamini wakijitokeza, zawadi zikawekwa na waandaaji wakaweka utaratibu wa kutambua wachezaji wenye uwezo, mashindano hayo yanaweza kuwa sehemu ya mfumo wa kukuza vipaji.
Faida yake haitakuwa kwa wachezaji pekee pia vilabu vya Ligi Kuu Tanzania Bara na madaraja mengine vinaweza kupata chanzo kingine cha wachezaji, badala ya kutegemea zaidi usajili wa wachezaji kutoka maeneo mengine hususani nje ya nchi, jambo hilo linaweza kupunguza baadhi ya gharama za utafutaji na usajili, huku likitoa nafasi kwa vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini kupitia tasnia ya soka.
Mwisho wa yote, kipaji hakipaswi kupimwa kwa mahali mchezaji anapotoka , Viwanja vya mitaani vinaweza kuwa na wachezaji wenye uwezo ambao wanahitaji tu nafasi ya kuonekana na mfumo wa kuwaendeleza.
Ikiwa Tanzania itaweka nguvu zaidi katika kuzunguka maeneo mbalimbali na kuibua vipaji vilivyopo, badala ya kusubiri vipaji hivyo vifike kwenye vituo vikubwa vya soka, huenda ikafungua njia mpya ya kupata kizazi cha wachezaji kutoka mitaani hadi kwenye ngazi ya juu ya soka.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment