Miaka ishirini bado wanaitafuta Ballon d’Or


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Tangu Ballon d’Or ilipoanzishwa mwaka 1956, imekuwa ni jambo la kawaida kuona tuzo hiyo ikienda kwa viungo na washambuliaji. Mabeki wamekuwa wakipambana kuingia kwenye orodha hiyo, lakini ni wachache sana waliofanikiwa kuinyanyua.

Mpaka sasa, mabeki watatu pekee ndio wamewahi kutwaa tuzo hiyo, Wa kwanza ni Franz Beckenbauer, aliyefanikiwa kushinda mara mbili, mwaka 1972 na 1976, wakati akiichezea Bayern Munich, Miaka 20 baadaye, Matthias Sammer aliendeleza historia hiyo mwaka 1996 akiwa Borussia Dortmund.

Kisha mwaka 2006, Fabio Cannavaro akawa beki wa tatu kutwaa tuzo hiyo akiwa Real Madrid. Cannavaro aliingia kwenye ushindani huo baada ya kuiongoza Italia kutwaa Kombe la Dunia mwaka huo.

Tangu Cannavaro aliposhinda, hakuna beki mwingine aliyefanikiwa kuchukua Ballon d’Or. Hata hivyo, baadhi wamewahi kusogea karibu, akiwamo Virgil van Dijk, aliyemaliza nafasi ya pili mwaka 2019.

Sasa macho yanaelekezwa kwa kizazi kipya cha mabeki, Kwenye orodha ya Ballon d’Or ya 2026 wapo Pau Cubarsí wa Barcelona, Gabriel na Saliba wa Arsenal, Nuno Mendes na Achraf Hakimi wa Paris Saint-Germain na cucurella wa Real Madrid, ambao wameingia kwenye orodha ya wanaowania tuzo hiyo.

Kwao, changamoto si kuingia kwenye orodha pekee, bali kuvuka hatua ambazo mabeki wengi waliowatangulia walishindwa kuzivuka.

Historia inaonyesha kuwa si rahisi kwa beki kutwaa Ballon d’Or, lakini uwepo wa majina hayo kwenye orodha ya mwaka huu unaacha swali je, baada ya miaka 20 tangu Cannavaro atwae tuzo hiyo, Dunia inaweza kushuhudia beki mwingine akiandika jina lake kwenye historia ya Ballon d’Or?

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments