Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Baada ya msimu wa 2025/26, Tottenham Hotspur walinusurika kushuka daraja katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu England baada ya kuifunga Everton bao 1-0. Matokeo hayo yaliwafanya kumaliza msimu katika nafasi ya 17 wakiwa na alama 41.
Kwa timu ambayo kwa miaka kadhaa imekuwa ikitajwa miongoni mwa kundi la Big Six nchini England, msimu huo ulionekana kama anguko ama kuteleza, hata hivyo, mwanzo wa msimu mpya ulitoa matumaini ya kuona Spurs wakirejea kwenye ushindani wa juu.
Usajili uliofanyika kabla ya msimu kuanza ulionekana kutoa ishara kwamba klabu ilikuwa ikijenga kikosi kwaajili ya kufuta matokeo ya msimu uliopita, na mashabiki walikuwa na matarajio ya kuona timu hiyo ikirejea katika nafasi za juu kwenye msimamo.
Lakini isivyo bahati baada ya michezo mitano, mambo yamekwenda tofauti Spurs wamepoteza michezo mitatu na kutoka sare michezo miwili, hivyo kuvuna alama mbili na kuburuza mkia kwenye msimamo wa ligi.
Msimamo huo unaifanya Spurs kuendelea kuwa karibu na eneo la kushuka daraja, jambo ambalo linaongeza presha kwa timu ambayo kwa kipindi kirefu ilikuwa ikipambania nafasi za juu na kushiriki michuano ya Ulaya.
Kutoka kuwa sehemu ya Big Six hadi kupambana katika eneo la chini la msimamo ni anguko kwa timu, hata hivyo, soka limewahi kuonyesha kuwa jina la klabu pekee haliwezi kuhakikisha matokeo klabu inahitaji kikosi, benchi la ufundi na maamuzi yanayoendana na hali iliyopo.
Katika hali hiyo, benchi la ufundi linaloongozwa na Roberto De Zearb lina kazi ya kutafuta suluhisho kabla ya mambo hayajaanza kuharibika zaidi.
Moja ya mambo yanayoweza kuangaliwa ni namna ya kutumia wachezaji waliopo kwenye kikosi. Miongoni mwao ni Richarlison, mshambuliaji mwenye uzoefu wa Ligi Kuu England ambaye kwa sasa hapati nafasi ya kucheza sio kwa sababu hana kiwango bali ni kocha kaamua kutomtumia kwa sababu zake binafsi.
Kwa hali ilivyo, Spurs wanahitaji kuangalia kila chaguo walilonalo katika safu ya ushambuliaji huku Kumtumia Richarlison pale ambapo benchi la ufundi linaona anaweza kusaidia ni moja ya mambo yanayoweza kujaribiwa katika kutafuta matokeo.
Hili si suala la kumlazimisha kocha kubadili falsafa yake, bali ni kuangalia kikosi kilichopo na kutumia wachezaji wanaoweza kutoa suluhisho katika kipindi ambacho timu inahitaji alama.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment