Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Mwanakwetu anauliza kabla ya darasa kulikuwa na mchaka mchaka , uko wapi Leo?. Kwa miaka kadhaa nyuma angalau mara mbili kwa wiki, wanafunzi walipata muda wa kutoka darasani, kukimbia pamoja na kuimba nyimbo zilizobeba ujumbe kuhusu uzalendo, afya, nidhamu na mambo mbalimbali ya kijamii.
Mbali na kuwapa wanafunzi muda wa kufanya mazoezi, mchaka mchaka ulihusisha nyimbo zilizokuwa na ujumbe kuhusu historia na misimamo ya Taifa. Baadhi ya nyimbo zilikumbusha wanafunzi misukosuko ambayo Tanzania ilipitia, ikiwemo vita dhidi ya Uganda wakati wa utawala wa Idi Amin.
Mfano wa nyimbo hizo ni ule uliokuwa na maneno, “Idi Amin akifa, mimi siwezi kulia, nitamtupa Kagera awe chakula cha mamba.” Nyimbo kama hizi zilitumika pia kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu historia ya Taifa na kuwakumbusha umuhimu wa kulinda nchi.
Hata hivyo, utamaduni huo kwa kiasi kikubwa haupo tena katika shule nyingi, Wanafunzi hutumia muda mwingi darasani wakisoma masomo yao, huku nafasi ya mazoezi ya pamoja na shughuli zinazohusisha ujumbe wa kijamii ikiwa ndogo.
Hapo ndipo mchaka mchaka unapoweza kurejeshwa, si kama zoezi la kukimbia pekee, bali kama sehemu ya elimu ya mwanafunzi. Shule zinaweza kutumia muda huo kuwaunganisha wanafunzi katika mazoezi huku wakipata ujumbe unaohusiana na maisha yao ya kila siku.
Kwa mfano, nyimbo zinazotumika wakati wa mchaka mchaka zinaweza kubeba ujumbe kuhusu kujikinga dhidi ya ukatili wa kijinsia, matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa, usafi wa mazingira, nidhamu na masuala mengine yanayowahusu vijana ikiwemo kupinga kwa vitendo vya ushoga ambavyo vimeshika kasi nchini.
Pamoja na hilo, shule zinaweza kutumia mchaka mchaka kuendeleza uzalendo na kuwafundisha wanafunzi historia ya Tanzania kupitia nyimbo na ujumbe unaoeleweka kwa kizazi cha sasa.
Elimu haiishii darasani pekee , mwanafunzi anahitaji pia muda wa kufanya mazoezi, kushirikiana na wenzake na kupata elimu inayohusiana na mazingira anayokutana nayo katika maisha yake.
Kwa hiyo, kurejesha mchaka mchaka mashuleni kunaweza kuwa sehemu ya kuongeza mazoezi ya mwili na wakati huo huo kutumia michezo, nyimbo na ujumbe kuwafundisha wanafunzi masuala yanayohusu afya, uzalendo, historia na maisha ya jamii.
Mchaka mchaka ulikuwa na nafasi yake katika shule. ni wakati wa kuangalia namna ya kuurudisha katika mfumo wa elimu wa sasa.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment