Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Katika soka, si kila mwanzo huenda kama ulivyopangwa wakati mwingine matarajio hujengwa kutokana na mafanikio ya jana, lakini msimu mpya unapofika mambo huanza kwa sura tofauti.
Hali hiyo ndiyo inayomkabili kocha wa Manchester United, Michael Carrick, ambaye baada ya kuiongoza timu katika nusu ya pili ya msimu uliopita alipewa nafasi ya kuendelea kuwa kocha wa kudumu.
Carrick aliichukua United katikati ya msimu wa 2025/26 na kuibadilisha hali ya timu, akaiwezesha kumaliza katika nafasi za juu na kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. Matokeo hayo yaliifanya klabu pamoja na mashabiki kuona kuwa huenda amekuwa mtu sahihi wa kupewa jukumu la kuanza kujenga timu kwa muda mrefu.
Lakini msimu wake wa kwanza akiwa kocha wa kudumu umeanza tofauti na matarajio ya Wengi, baada ya michezo minne ya Ligi Kuu England, United imekusanya pointi nne, ikishinda mchezo mmoja, kutoka sare mmoja na kupoteza miwili, Kama hiyo haitoshi, timu hiyo pia imeondolewa kwenye Carabao Cup baada ya kufungwa mabao 3-2 na Brighton, katika mchezo ambao United ilikuwa imeanza kwa kuongoza 2-0.
Matokeo hayo yanaweza kuibua maswali kuhusu Carrick, hasa kwa sababu matarajio yalikuwa makubwa baada ya kile alichokifanya msimu uliopita.
Hata hivyo, huu bado ni mwanzo wa safari, Carrick sasa yupo katika mazingira tofauti na yale aliyokutana nayo alipokuja katikati ya msimu bado ana nafasi ya kupanga kikosi, kujenga mfumo wake na kuwafanya wachezaji waelewe kile anachotaka. Mambo hayo yanahitaji muda, hasa kwa kocha anayeanza msimu wake wa kwanza akiwa na jukumu la kudumu kama kocha.
Hiyo haimaanishi kuwa matatizo yaliyopo yapuuzwe, United inapaswa kurekebisha namna inavyodhibiti michezo na kuhakikisha haipotezi faida kama ilivyotokea dhidi ya Brighton Lakini kumhukumu Carrick kwa michezo michache pekee kunaweza kuwa mapema.
Uongozi ulimpa nafasi kwa sababu ya kazi aliyofanya msimu uliopita, Sasa kinachohitajika ni kuona kama ataweza kutumia muda huo kujenga timu inayoweza kutoa matokeo kwa kipindi kirefu.
Katika soka, matokeo yanaweza kwenda tofauti na matarajio, Cha muhimu ni namna timu inavyorejea baada ya mwanzo huo.
Kwa Carrick, safari bado ni ndefu, Msimu ndio umeanza, na muda utatoa picha kubwa zaidi kuhusu kama uamuzi wa Manchester United wa kuendelea naye utaanza kuzaa matokeo waliyoyatarajia.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment