Kuna maisha baada ya masomo, michezo mashuleni ipewe kipaumbele


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports 

Kwa miaka ya nyuma, shule zilitenga siku maalumu kwa ajili ya michezo, jambo lililowapa wanafunzi nafasi ya kushiriki katika michezo mbalimbali kwa kuonyesha vipaji na kutumia muda wao nje ya masomo ya darasani katika viwanja mashuleni.

Siku hizo zilikuwa sehemu ya maisha ya shule, Wanafunzi walikutana kwenye viwanja, kushindana na kufurahia michezo, Kupitia mazingira hayo baadhi ya vipaji vilianza kuonekana na wanafunzi kupata nafasi ya kujenga uwezo wao katika michezo waliyoipenda.

Aidha, michezo iliimarisha mahusiano baina ya shule, Shule zilialikana katika michezo ya kirafiki, hali iliyowafanya wanafunzi kukutana na kujenga urafiki Katika baadhi ya maeneo, ushindani wa kimichezo baina ya shule ulikuwa sehemu ya utambulisho wa shule hizo.


Pia wanafunzi walipata nafasi ya kujikomaza kitaaluma kupitia shindano la "DEBATE" ambalo mara nyingi lilichukuwa nafasi kabla ya ushindani wa uwanjani , wanafunzi walikutana ulingoni kuchuana kitaaluma na kuonyesha uwezo wa kujenga na kutetea hoja, hakika ilivutia sana.

Siku za Jumatano na Ijumaa zilikua na nafasi katika ratiba za shule, Kila shule ilichagua siku ambayo ingetumia kwa ajili ya michezo, hivyo wanafunzi walipata muda wa kushiriki na kuonyesha uwezo wao.

Michezo pia ilitoa nafasi kwa wanafunzi ambao hawakuwa wakifanya vizuri kitaaluma kuonyesha uwezo wao katika eneo lingine, baadhi yao walijenga majina kupitia michezo na wengine kupata fursa za kuendeleza vipaji vyao.

Hata hivyo, kwa sasa michezo mashuleni imepungua, Wanafunzi wengi wanatumia muda mwingi darasani na baadhi yao huendelea na masomo hadi mwisho wa wiki kutokana na ratiba iliyopangwa na waalimu , hali hiyo inapunguza muda wa kushiriki michezo na kuendeleza vipaji miongoni mwa wanafunzi.


Wakati ambao michezo imekuwa sehemu ya ajira na imewapa vijana fursa za kujiajiri na kuajiriwa, shule zinapaswa kuwa moja ya maeneo ya msingi ya kutambua na kukuza vipaji hivyo kwa kutoa muda wa kutosha kwa wanafunzi ili waendeleze vipaji walivyo navyo kwa kuzingatia kuwa Kuna maisha baada ya shule.

Kwa hiyo, idara za elimu zinapaswa kushirikiana na taasisi za michezo kuweka ratiba na mazingira yatakayowapa wanafunzi nafasi ya kushiriki michezo. Hatua hiyo inaweza kusaidia kutambua vipaji mapema, huku michezo ikiendelea kuwa sehemu ya malezi na maendeleo ya mwanafunzi.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments