Kipaji cha mtoto hakipaswi kuwa gharama ya kuvumilia unyanyasaji katika michezo


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Ndoto ya mtoto kufanya vizuri katika michezo haipaswi kuwa sababu ya kupoteza utu, usalama na haki zake, Watoto wengi wana vipaji katika michezo mbalimbali na wana ndoto ya kufika mbali kupitia vipaji hivyo. Hata hivyo, nafasi zinazopatikana katika timu, vituo vya mafunzo na mashindano huwa chache ikilinganishwa na idadi ya watoto wanaohitaji fursa.

Katika mazingira hayo, baadhi ya watu wenye mamlaka katika michezo wanaweza kutumia nafasi zao vibaya kwa kuwashawishi au kuwanyanyasa watoto kingono kwa kisingizio cha kuwapa nafasi ya kucheza, kuchaguliwa kwenye timu au kusaidiwa kufikia hatua nyingine ya kimichezo.

Hili ni jambo linalopaswa kukemewa kwa sababu mtoto anayekwenda kwenye michezo anapaswa kupata nafasi ya kukuza kipaji chake, na si kukutana na mazingira yanayohatarisha utu na usalama wake.

UNICEF imeeleza kuwa watoto wanakabiliwa na aina mbalimbali za ukatili na unyanyasaji, huku mazingira ya michezo yakiwa miongoni mwa maeneo ambayo yanahitaji mifumo madhubuti ya ulinzi wa watoto , hii inaonyesha umuhimu wa kuhakikisha vituo vya michezo vinakuwa salama kwa watoto.


Kwa upande mwingine, wazazi na walezi wana nafasi kubwa katika ulinzi wa watoto wao, ni muhimu kufahamu vituo wanavyokwenda, watu wanaowafundisha na mazingira wanayokutana nayo wakati wa mazoezi au mashindano. Pia mtoto anapaswa kupewa nafasi ya kueleza changamoto anazokutana nazo bila kuogopa kulaumiwa.

Vituo vya michezo navyo vinapaswa kuwa na utaratibu wa kuwalinda watoto, kuwaelimisha makocha na wasimamizi kuhusu ulinzi wa mtoto na kuweka njia salama za kutoa taarifa endapo kuna vitendo vya unyanyasaji.

Fursa za michezo zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia uwezo na maendeleo ya mtoto, si kwa masharti yanayohusisha vitendo vya kingono au aina nyingine ya unyanyasaji.


Kipaji cha mtoto kinaweza kuwa mwanzo wa maisha yake ya mafanikio, lakini hakipaswi kuwa gharama ya kuvumilia unyanyasaji, Wazazi, walezi, jamii, viongozi wa michezo na mamlaka husika wanapaswa kusimama pamoja kuhakikisha mtoto anapata fursa ya kukuza kipaji chake huku akilindwa utu na usalama wake.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments