Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Mwanza inaweza kubaki bila timu katika Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa hali ya Pamba Jiji itaendelea kuwa kama ilivyo sasa. Jiji ambalo kwa muda mrefu limekuwa moja ya maeneo yenye historia katika soka nchini, sasa linaangalia timu yake ikipambana kuepuka kushuka daraja.
Pamba Jiji imeendelea kupata matokeo yasiyoridhisha katika michezo yake ya mwanzo ya msimu, hali iliyoifanya ibaki na alama moja baada ya michezo sita na kushika nafasi ya mwisho kwenye msimamo jambo ambalo linatengeneza msimu mgumu kwa klabu hiyo.
Hili si suala la Pamba Jiji pekee, bali linapaswa kuamsha mjadala kwa wadau wa soka jijini Mwanza kuhusu mwelekeo wa soka la eneo hilo.
Ukiangalia Arusha, kwa muda mrefu jiji hilo limekuwa likitafuta nafasi ya kuwa na timu katika Ligi Kuu , Sasa lina timu mbili zinazocheza ligi hiyo, TRA United na Fountain Gate, licha ya timu hizo kutokuwa na asili ya Arusha lakini zimehamishia makao yao jijini humo.
Mwanza yenyewe imekuwa na timu kadhaa zilizowahi kucheza Ligi Kuu, lakini zimeshindwa kujenga mwendelezo hapa Kuna Toto Africans imepotea kwenye ramani ya Ligi Kuu, Mbao FC nayo haipo, Alliance FC haipo na Gwambina FC pia haipo , Sasa Pamba Jiji ndiyo iliyobaki kubeba jina la Mwanza kwenye ligi hiyo.
Hapo ndipo swali linapoibuka, Mwanza inaelekea wapi katika soka la Tanzania?Tatizo haliwezi kuishia kwa kusema Pamba Jiji haipati matokeo bali Kinachohitajika ni kuangalia mfumo mzima wa usimamizi wa soka jijini, kwa sababu timu moja baada ya nyingine zimekuwa zikifika Ligi Kuu kisha kushindwa kujenga msingi wa kuendelea kuwepo kwenye ramani ya soka nchini.
Pamba Jiji sasa inahitaji hatua za mapema ili kujinusuru, Viongozi wa klabu, kwa kushirikiana na wadau wa soka jijini humo, wanapaswa kukaa pamoja na kutafuta njia ya kuimarisha timu kabla hali haijawa ngumu zaidi.
Mwanza ni moja ya miji yenye historia katika soka la Tanzania, Kupoteza nafasi yake kwenye Ligi Kuu hakutakuwa hasara kwa Pamba Jiji pekee, bali kutapunguza pia uwakilishi wa jiji hilo kwenye ligi ya juu nchini.
Kwa hiyo, wakati bado kuna nafasi ya kubadilisha mwelekeo, Pamba Jiji lazima ipambane kubaki Ligi Kuu, huku Mwanza ikianza upya kujenga mfumo utakaohakikisha kuwa timu zake haziishii kupanda na kushuka bila mwendelezo.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment