Hivi ndivyo jezi inapaswa kutumika ili kurejesha uzalendo na timu ya Taifa


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kwa miaka kadhaa sasa, katika shule na baadhi ya vyuo kumekuwa na utaratibu wa wanafunzi kuwa na sare maalumu za michezo ambazo huvaliwa siku za michezo na wakati mwingine wanafunzi huzitumia hata wanapokuwa nje ya muda wa masomo.

Hapa ndipo tunapoweza kujiuliza, kwa nini sare hizo zisitumike kujenga utamaduni wa kuipenda na kuiunga mkono timu ya Taifa, Taifa Stars?

Wizara yenye dhamana inaweza kuweka utaratibu ambao kila mwanafunzi anakuwa na jezi rasmi ya Taifa Stars kama sare yake ya michezo. Ikiwa hatua hii itaambatana na mpango mzuri wa uhamasishaji, inaweza kuwa njia mojawapo ya kuifanya Stars kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania.

Kuna msingi wa kisaikolojia unaoweza kuhusishwa na jambo hili unaojulikana kama "mere exposure effect" , nadharia hii inaeleza kuwa kadri mtu anavyokutana mara kwa mara na kitu fulani, ndivyo uwezekano wa kukizoea na kukipenda unavyoweza kuongezeka. Kwa hiyo, mwanafunzi anayekutana mara kwa mara na jezi yenye nembo na rangi za Taifa Stars anaweza kuijenga ndani yake hali ya kuiona timu hiyo kama sehemu ya maisha yake.

Kwa sasa changamoto moja inayojitokeza ni namna ya kuifanya Stars ibaki kwenye mawazo ya Watanzania hata pale ambapo hakuna mchezo, timu ya Taifa haiwezi kujenga mashabiki kwa siku za mashindano pekee bali inahitaji kuonekana, kuzungumzwa na kuwa sehemu ya maisha ya watu.

Kama kila mwanafunzi atakuwa na jezi rasmi ya Taifa Stars, faida ya kwanza itakuwa kuongeza matumizi na mauzo ya jezi hizo, badala ya jezi ya Taifa kuonekana zaidi siku ambazo timu inacheza, itaonekana shuleni, viwanjani, mitaani na kwenye shughuli mbalimbali za vijana.

Pili hatua hiyo inaweza kuongeza hamasa ya kuifuatilia timu, Mtoto anayekulia katika mazingira ambayo jezi ya Taifa ni sehemu ya sare yake ya michezo ana nafasi kubwa ya kuifahamu timu, wachezaji wake na mashindano inayoshiriki. Hapo Taifa Stars haitakuwa jina linalotajwa wakati wa mchezo pekee, bali timu ambayo mtoto amekuwa akiiona tangu akiwa mdogo.

Tatu, utamaduni huo unaweza kuenea kutoka kwa wanafunzi kwenda kwa jamii ,Wazazi, ndugu na watu wengine watakapoona watoto wao wakivaa jezi za Taifa Stars mara kwa mara, jezi hiyo inaweza kuanza kuchukuliwa kama sehemu ya utamaduni wa kitaifa na hatimaye kuvaa jezi ya Taifa hakutakuwa jambo la kusubiri siku ya mchezo pekee.


Nne, hatua hii inaweza kusaidia kujenga uzalendo. Shuleni ndipo mtoto anapojifunza mambo mengi kuhusu nchi yake, na michezo inaweza kutumika kama moja ya njia za kuufanya uzalendo huo uonekane katika vitendo, Jezi inaweza kuwa zaidi ya vazi la michezo, inaweza kuwa alama inayomkumbusha mwanafunzi kwamba Taifa Stars ni timu inayowakilisha Taifa.

Hata hivyo, matumizi ya jezi pekee hayatoshi, Inapaswa kwenda sambamba na programu ya kuifanya Taifa Stars kuwa timu inayopata nafasi kubwa katika uhamasishaji wa kitaifa. Wanafunzi wanapaswa pia kupewa muda wa kufahamu historia ya timu, wachezaji wake, mafanikio yake na umuhimu wa kuiunga mkono timu inayowakilisha Tanzania.

Jambo hili linaweza kuendelea hata kwa wanafunzi wanaopata nafasi ya kwenda Jeshi baada ya kumaliza kidato cha sita, Katika kipindi hicho cha mafunzo ya uzalendo na utaifa, wanafunzi wanaweza kutumia pia jezi za Taifa Stars katika shughuli zinazofaa, huku wakipatiwa elimu kuhusu uzalendo, wajibu wa raia na thamani ya kuilinda na kuiheshimu nchi yao.

Mwisho wa siku, tunahitaji kuanza kuiona Taifa Stars kama zaidi ya timu inayocheza mchezo iwe sehemu ya utamaduni wa Mtanzania.

Ikiwa mtoto atakua akivaa jezi ya Taifa Stars, akiiona kila mara, akizungumza kuhusu timu hiyo na kufundishwa kuiona kama sehemu ya utambulisho wa nchi yake, kuna uwezekano mkubwa wa Taifa Stars kupata kizazi kipya cha mashabiki.

Hivyo, kutumia jezi rasmi za Taifa Stars kama sare za michezo mashuleni si suala la mavazi pekee. Linaweza kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kujenga mashabiki, kuongeza mauzo ya jezi, kuimarisha uzalendo na kuifanya timu ya Taifa irudi kuwa sehemu ya maisha ya Watanzania.

0767915473.

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments