Dar es Salaam isiwe kimbilio pekee kwenye soka, vipaji vifuatwe mchangani

 

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kwa miaka mingi, Dar es Salaam imekuwa moja ya maeneo makubwa ambayo vijana wanaotamani kucheza soka la ushindani hukimbilia kutafuta nafasi Lakini kama Tanzania inataka kujenga mustakabali bora wa soka, ni wakati wa kuanza kuangalia pia nje ya Dar es Salaam.

Kila kona ya Tanzania kuna vijana wanaokua na ndoto za kuwa wachezaji wakubwa, Kutoka Iringa hadi Mwanza, Mbeya hadi Mtwara, wapo vijana wanaocheza kwenye viwanja vya mitaa bila kupata nafasi ya kuonekana na maskauti, kupata mafunzo bora au kujiunga na akademi zenye ushindani.

Tatizo si lazima liwe ukosefu wa vipaji, tatizo kubwa ni kutokuonekana kwao, Kwa maoni ya mwanakwetu klabu na maskauti wanapaswa kuongeza safari zao katika mikoa mbalimbali nchini na kupembua vipaji vilivyo bora katika soka, mchezaji hapaswi kulazimika kwenda Dar es Salaam ili kuthibitisha kuwa ana kipaji bali sehemu aliko anaweza kuonekana na kupewa fursa katika ulimwengu wa soka.


Mashindano ya shule, ligi za mitaa na michuano ya vijana yanaweza kuwa sehemu muhimu ya kugundua vipaji ikiwa yataandaliwa na kufuatiliwa kwa umakini na klabu za soka hapa nchini.

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikizungumzia maendeleo ya soka la vijana, Sasa ni wakati wa kutoka kwenye sehemu moja na kuzunguka maeneo mbali mbali na kuanza kutafuta vipaji kwa vitendo.

Mchezaji anayefuata wa kuibeba timu ya Taifa huenda asiwe anacheza katika akademi maarufu anaweza kuwa kijana anayepiga mpira kwenye uwanja mdogo, mbali na vituo vikubwa vya soka nchini. Vipaji vipo Kinachohitajika ni mfumo wa kwenda kuvifuata.


0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments