Bonas zitumike kulazisha klabu kufika hatua za juu za mashindano Afrika


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Kwa misimu kadhaa, timu za Tanzania zimekuwa zikipewa motisha ya fedha kuelekea michezo ya kimataifa, ambapo kiasi fulani kilitolewa kwa kila bao linalofungwa.

Mfumo huo ulipata nguvu baada ya Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuweka motisha kwa timu zinazoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ambapo Katika baadhi ya nyakati, bonasi kwa kila bao ilifikia Sh milioni tano hadi Milion 10, jambo lililoongeza hamasa ya wachezaji kutafuta mabao mengi na ushindi.

Hata hivyo, kwa msimu huu, mfumo huo unaweza kufanyiwa ubunifu kwa kuweka bonasi kubwa zaidi kwenye hatua ambazo timu za Tanzania zimekuwa zikishindwa kufika mara kwa mara.

Badala ya kuangalia mabao pekee, bonasi ziwekwe kwa malengo ya kufuzu nusu fainali, fainali na kutwaa ubingwa, Kila hatua iwe na kiwango chake cha fedha ili timu iwe na sababu ya kupambana katika kila mchezo hadi kufikia lengo lililowekwa.

Kwa mfano, timu ikifikisha robo fainali inaweza kupata bonasi fulani, ikifika nusu fainali kiasi kikaongezeka, huku kufuzu fainali na hatimaye kutwaa ubingwa kukiwa na bonasi kubwa zaidi.


Mfumo huo unaweza kufanya timu zisiridhike kufika hatua za awali na kuondolewa, bali ziweke malengo ya kusonga mbele zaidi, Kadiri hatua inavyokuwa kubwa, ndivyo bonasi inavyopaswa kuwa kubwa.

Hii pia inaweza kuendana na bonasi ya mabao ambayo imekuwa ikitumika, bao liendelee kuwa na motisha yake, lakini kufuzu hatua inayofuata kuwe na zawadi kubwa zaidi. Kwa kufanya hivyo, timu itakuwa na sababu mbili za kupambana kuongeza idadi ya mabao na kuhakikisha inafika hatua iliyowekewa bonasi.

Kwa miaka ya nyuma, Simba na Yanga zimewahi kufika hatua za juu katika mashindano ya CAF, lakini bado safari ya kutwaa mataji ya Afrika imekuwa ngumu. Hivyo, msimu huu mzigo wa motisha unaweza kuwekwa kwenye hatua ambazo hazijafikiwa kwa muda mrefu.

Nusu fainali isiwe mwisho wa safari, bali iwe hatua yenye bonasi inayolazimisha timu kutafuta fainali, Fainali nayo isiwe mafanikio ya mwisho, bali iwe njia ya kuelekea kwenye bonasi kubwa zaidi ya kutwaa taji.


Kwa hiyo, kama Tanzania inataka kuongeza ushindani wa timu zake kwenye mashindano ya Afrika, bonasi zisitazame bao pekee Ziweke malengo ya wazi ya kufika nusu fainali, fainali na kutwaa ubingwa.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.




0/Post a Comment/Comments