Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa kwenye mzunguko wa pili, mjadala kuhusu maamuzi ya waamuzi umeanza kubadilika baada ya matumizi ya teknolojia ya FVS, ambayo imewapa waamuzi nafasi ya kurejea matukio yenye utata kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Katika misimu iliyopita, makosa ya kibinadamu yalikuwa sehemu ya mchezo na wakati mwingine yaliibua malalamiko kutoka kwa klabu, hasa pale uamuzi ulipoathiri matokeo ya mchezo. Sasa, FVS imeongeza nafasi ya mwamuzi kupitia marejeo ya picha ili kupunguza uwezekano wa uamuzi usio sahihi.
Mabadiliko hayo yameonekana katika michezo ya msimu huu, huku Simba ikiwa miongoni mwa klabu zilizokutana na matokeo ya marejeo ya FVS. Katika michezo miwili, Simba imepata kadi nyekundu katika michezo mfululizo baada ya waamuzi kupitia matukio hayo kwa kutumia teknolojia hiyo.
Hali hiyo inaonyesha kuwa FVS haijawekwa kwa ajili ya kuwanufaisha klabu kubwa pekee, bali inatumika katika matukio yanayohitaji marejeo bila kuangalia ukubwa wa timu inayohusika.
Kabla ya matumizi ya teknolojia hiyo, uamuzi wa mwamuzi uliokuwa na utata ungeweza kuibua malalamiko kwa klabu na mashabiki, huku lawama nyingi zikielekezwa kwa waamuzi. Kwa sasa, mwamuzi ana nafasi ya pili ya kuliona tukio na kufanya uamuzi baada ya marejeo.
Kwa msimu huu, hilo linaweza kubadili pia namna malalamiko yanavyowasilishwa dhidi ya waamuzi. Badala ya kila kosa kuonekana kama kushindwa kwa mwamuzi, baadhi ya matukio yanaweza kutazamwa kupitia mchakato wa marejeo uliopo ndani ya mchezo.
Hivyo, kadri matumizi ya FVS yanavyoendelea katika Ligi Kuu, waamuzi wanaweza kuanza kuondoka kwenye presha ya malalamiko ya mara kwa mara, sio kwamba makosa yataisha kabisa, lakini nafasi ya kurekebisha baadhi ya maamuzi ndani ya mchezo imeongezeka.
Kwa maana hiyo, msimu huu unaweza kuwa mwanzo wa kipindi ambacho waamuzi wanaendalikizo ya malalamiko, huku teknolojia ikibeba sehemu ya jukumu la kuhakikisha maamuzi yanapitiwa kabla hayajawa chanzo cha mjadala mwingine nje ya uwanja.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment