Siasa isiwe chanzo Cha kudumaza michezo nchini



Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Soka limekuwa zaidi ya mchezo nchini Tanzania, Kwa miaka mingi limekuwa sehemu ya maisha ya Watanzania na moja ya maeneo yanayoweza kuwaunganisha watu wenye mitazamo tofauti tofauti na kuwaweka sehemu moja ndiyo maana suala la kuhusisha michezo na siasa linahitaji kuangaliwa kwa umakini.

Kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, kuhusu barua inayodaiwa kuandikwa kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ikiitaka kuahirisha au kuhamisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Tanzania. michuano ambayo itafanyika 2027 kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania , Kenya na Uganda.

“Ata juzi tumesema hawa majamaa wanatangaza kwamba kuna magaidi, tumeiandikia CAF kwamba waangalie upya mtazamo wenu na mambo mnayoyaleta hapa, kwa sababu hawa watu wanasema kuna magaidi hapa, sasa CAF wao wataamua AFCON ifanyike mahali kuna ugaidi au isifanyike.” amesema Heche.

Kauli hiyo inafungua mjadala. je, michezo inapaswa kuachwa nje ya mvutano wa kisiasa?

Kwa upande wa soka na michezo kwa ujumla, jibu ni ndiyo, Michezo imekuwa moja ya maeneo machache ambayo yanaweza kuwakutanisha Watanzania bila kuangalia tofauti zao za kisiasa ambapo Shabiki wa Yanga anaweza kusimama pamoja na shabiki wa Simba kuishangilia Taifa Stars wanasiasa wa vyama tofauti wanaweza kuwa upande mmoja wakati timu ya taifa au klabu Yao inapocheza , huo ndio umuhimu wa kuilinda soka isigeuke kuwa sehemu ya mapambano ya kisiasa.

kwa mfano Afcon , si tukio la chama cha siasa ni mashindano ya soka yanayowahusisha wachezaji, mashabiki, waandaaji na taasisi za michezo. Ikiwa Tanzania ni mwenyeji mmoja wapo , mjadala wake unapaswa kujikita katika maandalizi ya viwanja, usalama, miundombinu, usafiri, malazi na uwezo wa nchi kuandaa mashindano hayo ambayo yatalijenga taifa kiuchumi kupitia utalii na shughuli mbali mbali za biashara zitakazo kuwa zikiendelea wakati wa mashindano.

Hata pale ambapo kuna hoja kuhusu mazingira ya kisiasa au masuala mengine yanayoweza kuathiri mashindano, hoja hizo zinaweza kujadiliwa bila kufanya michezo kuwa uwanja wa mapambano ya kisiasa.


Tatizo linapotokea ni pale taasisi za michezo zinapoanza kutumika kama sehemu ya ujumbe wa kisiasa, Hapo ndipo michezo inapoweza kupoteza nafasi yake kwani wanamichezo wenyewe wanaitikadi zao , wote ni wanasiasa na huenda pia ni mahasimu kwenye masuala mengine, lakini kwenye michezo haya yote huwekwa pembeni na kufanya michezo ibaki kwenye nafasi yake ya kuwaunganisha watu wa kada zote.

Michezo husasani soka inahitaji uhuru wa kutosha ili liendelee kuwa eneo ambalo Watanzania wanakutana, Taifa linaposhangilia timu yake, tofauti za vyama, itikadi na mitazamo zinapaswa kubaki pembeni, Kinachobaki ni jezi ya timu au Taifa na matumaini ya ushindi.

Kwa hiyo, mjadala ulioibuliwa na kauli ya Heche haupaswi kuishia kwenye nani aliandika barua au nani alitakiwa kuiandika. Unapaswa kwenda kwenye swali kubwa zaidi la namna Tanzania inavyoweza kulinda nafasi ya michezo katika jamii.

Siasa zina nafasi yake, na michezo ina nafasi yake. Pale mipaka hiyo inapoheshimiwa, michezo itazidi kuendelea kuwa nyenzo ya umoja badala ya kuwa chanzo kingine cha mgawanyiko.

Na katika kipindi ambacho Tanzania inajiandaa kwa matukio makubwa ya soka, kulinda umoja huo ni muhimu kuliko kuifanya michezo kuwa sehemu ya mvutano wa kisiasa.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com



0/Post a Comment/Comments