Sababu ya lugha ya kiingereza kuendelea kutumika na waamuzi baada ya marejeo ya FVS


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Ligi Kuu ya Tanzania Bara imeanza kutumia Football Video Support (FVS) kama mfumo wa kusaidia waamuzi kufanya maamuzi kwenye matukio yenye utata, huku matumizi ya lugha ya Kiingereza katika kutoa maelezo ya maamuzi yakianza kujadiliwa na mashabiki.

Matumizi ya teknolojia hiyo yalianza rasmi Agosti 12, 2026, katika mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga uliochezwa Uwanja wa New Amaan, visiwani Zanzibar.

Matumizi ya FVS yamendelea baada ya mchezo huo, ambapo mfumo huo umetumika pia katika michezo mitatu ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyoanza Agosti 14, 2026, katika viwanja tofauti tofauti, Katika michezo hiyo, waamuzi walitumia lugha ya Kiingereza wakati wa kutoa maelezo ya maamuzi yaliyofanywa baada ya kupitia matukio kwa kutumia FVS.

Hatua hiyo imeibua mjadala kuhusu matumizi ya Kiingereza katika mawasiliano ya waamuzi wakati wa kutumia teknolojia hiyo, hasa katika ligi ambayo sehemu kubwa ya watazamaji wake ni Watanzania.

Hata hivyo, matumizi ya Kiingereza yanaweza kuwa na nafasi katika mazingira ya soka kutokana na ushiriki wa wachezaji na wadau kutoka mataifa mbalimbali Katika ligi yenye wachezaji wa ndani na wa kigeni, lugha hiyo inaweza kutumika kama lugha ya kuwaunganisha watu wenye lugha tofauti.

Aidha, Ligi Kuu ya Tanzania Bara inafuatiliwa na mashabiki kutoka nje ya Tanzania hivyo matumizi ya Kiingereza katika maelezo ya maamuzi yanaweza kuwasaidia watazamaji hao kuelewa kinachoendelea wakati mwamuzi anapofanya uamuzi kwa kutumia FVS badala ya kutumia lugha ambayo inaeleweka na baadhi ya wahusika.

Pamoja na hilo, sheria na taratibu za soka la kimataifa huwasilishwa kwa Kiingereza hivyo, matumizi ya lugha hiyo katika kueleza maamuzi ya mwamuzi yanaendana na lugha inayotumika katika mawasiliano ya kimataifa kuhusu sheria za mchezo.

Kwa upande mwingine, matumizi ya FVS yanahitaji waamuzi kuwa na uwezo wa kueleza uamuzi wao kwa lugha inayoeleweka na kwa kutumia istilahi sahihi za soka hii ni muhimu kwa sababu maelezo ya mwamuzi yanapaswa kueleza kwa ufupi sababu ya uamuzi uliofanywa baada ya kupitia tukio.

Kwa msingi huo, matumizi ya Kiingereza katika FVS ni sehemu ya mfumo wa mawasiliano unaoendana na mazingira ya soka la kimataifa Jambo la msingi ni kuhakikisha waamuzi wanatumia lugha hiyo kwa usahihi na kutoa maelezo yanayoeleweka kwa wafuatiliaji.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments