Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Katika soka la kisasa kusajili wachezaji ni sehemu muhimu ya kujenga kikosi chenye ushindani, Klabu inaponyimwa haki hiyo, hujikuta ikikabiliwa na changamoto za kiufundi, kifedha na kiutawala ambazo zinaweza kuathiri mipango yake.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limeiwekea klabu ya Yanga Africans marufuku ya kusajili wachezaji wapya kwa madirisha matatu mfululizo, huku adhabu hiyo ikianza kutumika rasmi Agosti 5, 2026, kufuatia migogoro ya kifedha pamoja na ukiukwaji wa kanuni za usajili.
Yanga si klabu pekee iliyochukuliwa hatua hiyo Orodha ya FIFA pia inajumuisha Chippa United ya Afrika Kusini, Al Dahra FC ya Libya, US Monastir ya Tunisia, pamoja na klabu za Tanzania ambazo ni Dodoma Jiji FC, Fountain Gate FC na Kengold SC.
Kwa mujibu wa utaratibu wa FIFA, marufuku ya usajili hutolewa pale klabu inaposhindwa kutekeleza wajibu wake wa kifedha au kukiuka taratibu za usajili wa wachezaji, adhabu hiyo huzuia klabu kusajili wachezaji wapya hadi pale itakapotekeleza masharti yaliyowekwa na kuondolewa kwenye orodha ya waliozuiwa kufanya usajili.
Kwa Yanga, adhabu hii inaweza kuathiri mipango ya kuimarisha kikosi ikiwa haitatatua sababu zilizosababisha hatua hiyo. Wachezaji waliopo wanaweza kuendelea kuitumikia klabu, lakini usajili wa nyongeza utasubiri hadi marufuku itakapoondolewa.
Sasa jukumu kubwa lipo kwa uongozi wa klabu kushughulikia migogoro iliyopo na kukamilisha taratibu zote zinazohitajika ili kurejesha haki ya kufanya usajili, hatua hizo zitakuwa muhimu katika kuhakikisha klabu inaendelea kutekeleza mipango yake ya mashindano ya ndani na kimataifa bila vikwazo vya usajili.
Tukio hili pia linatoa funzo kwa klabu nyingine kuhusu umuhimu wa kuzingatia kanuni za usajili na kutimiza wajibu wa kifedha kwa wakati, ili kuepuka adhabu zinazoweza kuathiri maendeleo ya timu na ushindani wake.
0767915474,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment