Nguvu ya mashabiki kwenye mafanikio ya vilabu

Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Katika soka la kisasa, mafanikio ya timu hayaamuliwi na kiwango cha wachezaji au mbinu za makocha pekee bali Mashabiki pia ni sehemu ya mchakato huo, Kila mchezo unapochezwa uwepo wao huathiri mazingira ya mchezo, huongeza ari kwa wachezaji na huchangia taswira ya ushindani wa timu.

Kwa muda mrefu, mchango wa mashabiki ulionekana kupitia ushangiliaji wao viwanjani, hata hivyo, tafiti zilizofanyika katika miaka ya karibuni zimeonyesha kuwa mchango huo unaonekana pia kwenye matokeo ya michezo, katika Kipindi cha UVIKO-19 kilitoa nafasi ya kulinganisha michezo iliyochezwa mbele ya mashabiki na ile iliyochezwa kwenye viwanja visivyo na watazamaji.

Utafiti uliochapishwa mwaka 2024 katika jarida la Soccer & Society ulibaini kuwa timu za nyumbani zilipata alama chache zilipocheza bila mashabiki aidha, tafiti zilionyesha kuwa faida ya kucheza nyumbani ilipungua na waamuzi walitoa maamuzi tofauti na yale yaliyokuwa yakionekana wakati viwanja vilikuwa na mashabiki ambapo hali hiyo ilionyesha kuwa uwepo wa mashabiki una nafasi katika mazingira ya ushindani wa mchezo.

Mbali na matokeo ya uwanjani, mashabiki wana mchango katika uchumi wa klabu, Mapato yanayotokana na tiketi, mauzo ya jezi na bidhaa nyingine pamoja na mikataba ya udhamini huongezeka pale ambapo klabu inaungwa mkono na idadi kubwa ya mashabiki huku Kadiri uwanja unavyojaa wakati wa mchezo, ndivyo klabu inavyopata nafasi ya kuongeza mapato na kuvutia wadhamini.


Kwa upande wa wachezaji, mashabiki huwapa sababu ya kupambana hadi dakika ya mwisho huku Ushangiliaji wao uki ongeza ari wakati timu inapokuwa nyuma kwa mabao au inapohitaji kulinda ushindi, hivyo hivyo uwepo wa mashabiki huufanya mchezo kuwa na ushindani unaowavutia wachezaji, makocha na watazamaji.

Hali hiyo inaonekana pia katika soka la Tanzania, michezo inayowakutanisha Simba, Yanga na Azam mara nyingi huvutia idadi kubwa ya mashabiki uwepo wao huongeza hamasa ya mchezo na kuifanya ligi ivutie wadhamini, vyombo vya habari na wadau wengine wa soka. Hata hivyo, mchango huo unapaswa kuambatana na nidhamu ili kuzuia vurugu, matumizi ya lugha zisizofaa na vitendo vinavyoweza kuathiri usalama wa mchezo.

Kutokana na hali hiyo, viongozi wa klabu wanapaswa kuendelea kuboresha huduma kwa mashabiki, kuimarisha usalama viwanjani na kujenga mazingira yanayowahamasisha kuhudhuria michezo ikiwemo kupata matokeo mazuri , hatua hizo zinaweza kuongeza mapato ya klabu na kuimarisha ushindani wa ligi.

Kwa ujumla, mafanikio ya timu hayategemei maandalizi ya kikosi pekee, Mashabiki ni sehemu ya mfumo unaochangia ushindani wa timu ndani na nje ya uwanja pale Wanapokuwa karibu na timu yao, huongeza nguvu ya ushindani, huimarisha mapato ya klabu na huchangia maendeleo ya soka kwa ujumla.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments