Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Michezo ni afya, michezo ni burudani, lakini zaidi ya hapo, michezo ni umoja. Watu hukutana uwanjani kwa lengo la kushindana, kuonyesha uwezo na kutafuta ushindi, lakini ushindani huo haupaswi kuondoa utu na usalama wa mshiriki mwingine.
Mchezaji anapoingia uwanjani anapaswa kuelewa kuwa anayekabiliana naye ni mpinzani wa mchezo, si adui wa maisha hivyo, kila mchezaji ana wajibu wa kulinda afya ya mwenzake kama anavyolinda afya yake mwenyewe.
Katika michezo, migongano inaweza kutokea kupitia Kasi ya mchezo, harakati za wachezaji na mazingira ya ushindani vinaweza kusababisha mchezaji kuanguka au kupata jeraha ambapo hizo ni sehemu ya hatari zinazoweza kujitokeza katika michezo, Lakini tofauti ipo kati ya jeraha linalotokea kwa bahati mbaya na kitendo cha kumuumiza mpinzani kwa makusudi.
Mchezo unapofika katika hatua ambayo mchezaji anaona ni sahihi kumuumiza mwenzake ili kupata faida, maana ya michezo inapotea na panakuwa hakuna utu tena, Ushindi unaopatikana kwa kumuumiza mwingine hauwezi kuwa na thamani sawa na ushindi unaopatikana kwa uwezo, nidhamu na ushindani wa haki.
Jambo hili halihusu mpira wa miguu pekee bali Pia Katika netball, basketball, volleyball, handball na michezo mingine, wachezaji hukutana kwa karibu na wakati mwingine migongano hutokea Kwa sababu hiyo kila mmoja anatakiwa kucheza kwa kuzingatia sheria na usalama wa mwenzake.
Mchezaji akimwangusha mwenzake kwa bahati mbaya, hilo linaweza kuwa sehemu ya mchezo Lakini pale anapolenga kumuumiza, anakuwa ameongeza hatari ambayo haikupaswa kuwepo, Jeraha moja linaweza kumtoa mchezaji nje ya uwanja kwa muda mrefu, kuathiri kipato chake na hata kuvuruga mipango yake ya maisha.
Nyuma ya kila mchezaji kuna maisha mengine, Kuna familia, ndugu na watu wanaomtegemea. Mchezaji anaweza kuwa mzazi, mtoto, kaka, dada au mlezi wa mtu mwingine iwapo Jeraha kubwa likimkumba linaweza kuathiri zaidi ya mtu aliyelipata na kuacha athari kwa watu wanaomzunguka.
Pia, kila mchezaji ana ndoto, mwingine anacheza kwa ajili ya kujenga taaluma, mwingine mazoezi, mwingine anatafuta nafasi ya kuiwakilisha timu yake ya taifa, huku mwingine akitumia kipaji chake kama njia ya kujenga maisha. Kitendo cha kumuumiza kwa makusudi kinaweza kuvuruga safari hiyo.
Ndiyo maana michezo inahitaji ushindani wenye mipaka, Kupambana kwa ajili ya ushindi ni sehemu ya mchezo, lakini kulindana ni sehemu ya utu wa mchezo, mchezaji anapaswa kutafuta kumshinda mpinzani wake kwa uwezo wa kimchezo, si kwa kumtoa kwenye mchezo kupitia jeraha.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.




Post a Comment