Mashaka yamekuwa kweli, Mfalme wa soka aachia kiti


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Mashaka ya Lionel Messi kuhusu kuendelea na soka la kimataifa yamekuwa kweli baada ya nyota huyo kutangaza kustaafu kuichezea Argentina, akihitimisha safari yake ya zaidi ya miaka 20 katika timu hiyo.

Messi alifikiria uamuzi huo siku chache baada ya kifo cha baba yake, Jorge Messi, ambaye alifariki Agosti 8 akiwa na umri wa miaka 68.

Kifo hicho kilimfanya Messi kuanza kujiuliza kuhusu mustakabali wake katika soka, baada ya kueleza kuwa alikuwa na mashaka kama angeendelea kucheza kwa muda mrefu na hatimaye ameamua kufanya maamuzi aliyokuwa akifikiria.


“Sijui nitafanya nini bila wewe, sijui nitaendeleaje. Nimecheza mpira tu na sasa nina mashaka kama nitaendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu zaidi,” Messi alisema katika ujumbe wa kumuaga baba yake.

Nyota huyo pia alieleza kuwa alikuwa amefanya uamuzi wa kustaafu muda mfupi baada ya Argentina kupoteza fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Hispania, lakini kifo cha baba yake kiliongeza msukumo wa kukamilisha uamuzi huo.

Katika ujumbe wake wa kutangaza kustaafu, Messi amesema:

“Ulikuwa uamuzi ulioniumiza na bado unauma sana moyoni, lakini ninaelewa kuwa wakati umefika.”

Messi ameichezea Argentina kwa zaidi ya miaka 20, akianza safari yake ya timu ya taifa mwaka 2005, Katika kipindi hicho, amecheza mechi 207 na kufunga mabao 125.

Mafanikio makubwa zaidi ya Messi akiwa na Argentina yalikuja mwaka 2022 alipoliongoza taifa hilo kushinda Kombe la Dunia nchini Qatar , Pia alisaidia Argentina kushinda Copa América mwaka 2021 na 2024.


Katika ujumbe wake wa kuaga, Messi amesema ametoa kila alichokuwa nacho kwa ajili ya timu ya taifa.

“Ninakuapia kwamba siku zote nilitoa kila nilichokuwa nacho, si katika miaka ya hivi karibuni tu tuliposhinda kila kitu, bali hata kabla ya hapo. Siku zote nilipambana na kutoa kila nilichokuwa nacho kwa ajili ya jezi hii, ili kuwaletea furaha na kuwafanya mjivunie kuwa Waargentina kupitia soka.”

Kustaafu kwa Messi kunahusu timu ya taifa pekee, kwani ataendelea na soka la klabu akiwa na Inter Miami ya Marekani.


Kwa Argentina, uamuzi huo unafunga ukurasa wa mmoja wa wachezaji waliobeba timu hiyo kwa zaidi ya miongo miwili, huku kizazi kipya kikipewa nafasi ya kuendeleza safari ya taifa hilo.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments