Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Sekunde chache zinaweza kubadili kila kitu ndani ya ulingo wa ngumi, bondia anaweza kuwa bado amesimama, mashabiki wakitaka pambano liendelee, lakini ghafla taulo likatupwa kutoka kona yake, watu wengi hulichukulia tukio hilo kama ishara ya kukubali kushindwa lakini Kwa wanaoufahamu mchezo huo kutupa taulo ni uamuzi unaoweka usalama wa bondia mbele ya matokeo ya pambano.
Ngumi ni miongoni mwa michezo inayoruhusu ushindani wa moja kwa moja kati ya mabondia wawili. Kutokana na mazingira hayo, sheria za mchezo zimeweka taratibu zinazolenga kuhakikisha pambano linaendeshwa bila kuhatarisha maisha ya washiriki ambapo moja ya taratibu hizo ni haki ya kona ya bondia kusimamisha pambano kwa kutupa taulo.
Katika mchezo wa ngumi, taulo hutupwa na kocha au mmoja wa wasaidizi wa bondia pale wanapotathmini kuwa bondia wao hawezi kuendelea kupigana kwa usalama, uamuzi huo unaweza kufikiwa baada ya kuona bondia amepokea kichapo kibaya na kupelekea majeraha mabaya na kushindwa kujibu mashambulizi au ameonyesha dalili zinazoashiria kuwa kuendelea kunaweza kuongeza hatari na madhara.
Taulo linapotupwa, mwamuzi husimamisha pambano mara moja Kisha ushindi hutolewa kwa bondia wa upande mwingine kwa Technical Knockout (TKO), hii ni kwa sababu pambano limekatishwa na kona ya mpinzani,l.
Jukumu la kona haliishii kutoa maelekezo kati ya raundi na raundi wakati wa pambano bali Pia ina wajibu wa kufuatilia hali ya bondia wake kuanzia mwanzo hadi mwisho wa pambano. Endapo Kona itaona uwezo wa bondia wa kujilinda umepungua au afya yake ipo hatarini, inaweza kuchukua uamuzi wa kutupa taulo hata kama bondia mwenyewe anatamani kuendelea.
Mbali na kona, mwamuzi na daktari wa pembeni ya ulingo pia wana mamlaka ya kusimamisha pambano endapo watabaini kuwa kuendelea kwa pambano kunaweza kuhatarisha afya ya bondia, hii inaonyesha kuwa sheria za ngumi zinatanguliza usalama wa washiriki kuliko matokeo ya pambano.
Katika historia ya ngumi, kumekuwa na matukio mengi ambayo kutupa taulo kumezuia mabondia kupata majeraha makubwa ingawa hatua hiyo huleta ushindi kwa mpinzani, mara nyingi huwapa mabondia nafasi ya kupata matibabu na kurejea tena ulingoni baada ya kupona.
Ndiyo maana ndani ya mchezo wa ngumi, kutupa taulo hakupaswi kutafsiriwa kama ishara ya udhaifu au kukata tamaa bali ni uamuzi unaozingatia sheria za mchezo, ushauri wa wataalamu wa kona na wajibu wa kulinda afya ya bondia.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.

Post a Comment