Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara inaendelea, lakini idadi ya mashabiki wanaofika viwanjani katika baadhi ya michezo bado ni ndogo, hali hiyo inaonekana zaidi kwenye michezo ambayo hazihusishi Simba na Yanga, huku timu mwenyeji zikipoteza fursa ya kupata mapato kupitia mauzo ya tiketi.
Kwa mfumo wa mapato ya milangoni, timu mwenyeji hunufaika na mapato ya mchezo, hata hivyo iwapo mashabiki hawajitokezi kwa wingi klabu hupoteza sehemu ya mapato ambayo ingeweza kusaidia katika uendeshaji wa timu.
Moja ya sababu inayoweza kuchangia hali hiyo ni upangaji wa muda na siku za michezo, baadhi ya michezo huchezwa nyakati ambazo mashabiki wengi bado wako kazini au wanaendelea na majukumu yao ya kila siku. Michezo inayochezwa katikati ya wiki pia huathiri mahudhurio kwa sababu sehemu kubwa ya mashabiki huwa kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa upande mwingine, matokeo ya timu yanaweza kuwa sababu ya mashabiki kwenda au kutokwenda uwanjani, hata hivyo, hali ya sasa inaonyesha kuwa matokeo mazuri pekee hayatoshi kuongeza mahudhurio kwani baadhi ya timu zimekuwa na matokeo mazuri lakini bado hazijafanikiwa kuvuta mashabiki wengi, huku Simba na Yanga zikiwa na idadi kubwa zaidi ya wafuasi, ingawa hata kwao mahudhurio yameanza kushuka.
Suluhisho linaweza kuanzia kwa mashabiki wenyewe, Kwenda uwanjani hakupaswi kutegemea ushindi pekee. Mpira unaweza kuwa sehemu ya burudani na mtoko wa familia, marafiki au jamii, huku mashabiki wakijenga utamaduni wa kuzisapoti timu za maeneo yao.
Wakati huohuo, Bodi ya Ligi na warusha matangazo wanapaswa kuangalia upya upangaji wa ratiba, michezo inaweza kupangwa zaidi katika muda ambao watu wamemaliza majukumu yao ya kila siku, kwa mfano kuanzia saa 10 jioni na zaidi pale miundombinu ya uwanja inaporuhusu.
Kuongeza mashabiki viwanjani kutahitaji ushirikiano wa klabu, waandaaji wa ligi, warusha matangazo na mashabiki, Ligi ikiwa na mashabiki wengi uwanjani, klabu zinaweza kuongeza mapato, huku mchezo wenyewe ukipata mazingira yanayowavutia zaidi wadau na wawekezaji.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com




Post a Comment