Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Mwanzo wa msimu wa soka Tanzania umejenga utamaduni mwingine ambapo Kwa kabla ya Simba , Yanga na baadhi ya vilabu kuanza safari ya msimu mpya, mashabiki hukutana kwenye matamasha yanayohusisha utambulisho wa vikosi, shughuli za kijamii, na burudani. utamaduni huo una historia yake na kwa upande wa Simba unahusishwa na wazo lililoanzishwa mwaka 2009.
Wakati huo, Hassan Dalali akiwa mwenyekiti wa Simba, kwa kushirikiana na katibu mkuu Mwina Kaduguda, waliasisi kuanzishwa kwa Simba Day ambapo Wazo lilikuwa kuunda siku ambayo klabu ingewakutanisha mashabiki na wanachama, kuitambulisha timu kuelekea msimu mpya na pia kupata fedha kwa ajili ya shughuli za klabu ikiwemo ujenzi wa uwanja wa Bunju na hapo ndipo msingi wa utamaduni unao onekana leo ulipoanzia.
Hata hivyo, kadiri miaka ilivyopita, Simba Day haikubaki katika lengo lake la awali, Viongozi waliokuja baada ya Dalali waliendelea na tamasha hilo na kuongeza shughuli mbalimbali, jambo lililolifanya liendelee kuwa sehemu ya ratiba ya klabu.
Utamaduni huo baadaye ukaingia upande wa pili wa ushindani, klabu ya Yanga ikiwa mpinzani wa jadi wa Simba, nayo iliona umuhimu wa kuwa na tukio linalowaleta pamoja mashabiki wake na klabu ambapo mwaka 2019, klabu hiyo ilianzisha Wiki ya Mwananchi, mfumo ambao haukuishia kwenye siku moja bali ulihusisha shughuli mbalimbali kabla ya kufikia siku ya kilele.
Kwa Simba huazimisha tukio hilo agosti 8, Kila mwaka huku Yanga wakifanya agosti 9 . Vilabu hivyo hutumia wiki Moja kabla ya siku ya kilele kwa kufanya shughuli mbali mbali za kijamii ikiwemo uchangiaji wa damu, kutembelea vituo vya afya na kutoa mahitaji kwa wahitahiji, jambo ambalo linazifanya siku hizo zisisalie tu kwenye soka bali kuvuka mipaka na kuingia kwenye kumbukumbu za wanajamii wanaoguswa au kufikiwa na vilabu hivyo Moja kwa moja ambapo mpaka sasa Simba wanatimiza mika 17 ya tamasha lao huku Yanga wakiwa na miaka nane.
Cha kufurahisha zaidi matamasha haya yamegeuka fursa kwa makundi mbali mbali nchini na nje ya nchi, wasanii wamekuwa sehemu ya shughuli hizo ambapo nao hupata kipato kwa kutumbuiza huku wajasilia mali nao wakipata chochote kwaajili ya kuendelea kuendesha maisha yao. Mabadiliko hayo yanaonyesha kwamba wazo la Dalali limepita zaidi ya malengo ya awali , tamasha ambalo lilianza kama njia ya kukusanya fedha na kuwaunganisha mashabiki limeendelea kuwa sehemu ya utambulisho wa klabu na soka la Tanzania Duniani.
Kwa upande mwingine, kuanzishwa kwa matamasha hayo kunafanya ushindani wa Simba na Yanga kuonekana hata nje ya uwanja huku ushindani huo sasa haupimwi kupitia matokeo ya michezo pekee, bali pia namna kila klabu inavyowafikia mashabiki wake na kushiriki katika shughuli za jamii.
Matamasha haya yameendelea kubadilika kutokana na mahitaji ya soka la kisasa Klabu zinahitaji mashabiki, mashabiki wanahitaji ukaribu na klabu zao, huku matukio kama haya yakitoa nafasi ya kujenga uhusiano huo ndiyo maana shughuli za kijamii zimekuwa sehemu ya ratiba kuelekea kilele cha matamasha.
Kwa Simba, msingi uliwekwa mwaka 2009 chini ya Hassan Dalali na viongozi wenzake. Kwa Yanga, wazo hilo lilipata mfumo wake kupitia Wiki ya Mwananchi kuanzia mwaka 2019, tangu hapo, matamasha haya yameendelea kuwa sehemu ya utamaduni wa vilabu hivyo huku baadhi ya vilabu nchini vikijaribu kuiga mfumo huo kuwa sehemu ya utamaduni wao.
Wazo lilianza kama tamasha la klabu na miaka ilivyopita likageuka kuwa utamaduni wa soka na sasa, mwanzo wa msimu kwa Simba na Yanga hauonekani mzuri bila matukio hayo, kwa yote haya ashukuriwe Hassan Dalali.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com






Post a Comment