Kutoka kuzuiwa Kombe la Dunia hadi kuandika historia Ulaya


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Alipaswa kuwa Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia 2026, lakini safari yake ilisimama kabla ya kufika uwanjani na miezi michache baadaye, Omar Artan kutoka Somalia alipewa nafasi nyingine ambayo ilimpeleka kwenye hatua ya historia ya soka la Ulaya na yeye binafsi.

Artan alikuwa miongoni mwa waamuzi wa FIFA walioteuliwa kuchezesha Kombe la Dunia 2026 lililofanyika kwa ushirikianao wa Marekani, Canada na Mexico, hata hivyo, hakuruhusiwa kuingia Marekani kutokana na sababu za kidiplomasia, hivyo akakosa nafasi ya kuchezesha katika mashindano hayo.

Pamoja na kutoshiriki kwenye mchezo wowote mwamuzi huyo alipata stahiki zilizokuwa zimetengwa kwa waamuzi walioteuliwa kushiriki Kombe la Dunia.

Baada ya kukosa nafasi hiyo, UEFA ilimpa jukumu jingine Juni 11, 2026, shirikisho hilo lilimtangaza kuwa mwamuzi wa UEFA Super Cup iliyochezwa Agosti 12 mjini Salzburg, Austria, kati ya Paris Saint-Germain na Aston Villa mchezo uliomalizika kwa PSG kushinda 2-1 na kutawazwa mabingwa wa kombe hilo.


Uteuzi huo ulimuingiza Artan katika historia ya UEFA Super Cup kwa kuwa mwamuzi wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kuchezesha mchezo huo na zaidi ya hapo, alifanya hivyo akiwa mwamuzi kutoka Somalia, taifa ambalo si mwanachama wa UEFA.

Hivyo, ndani ya muda mfupi, Artan alitoka kwenye kukosa nafasi ya kuchezesha Kombe la Dunia kutokana na kuzuiwa kuingia nchini Marekani hadi kupewa jukumu la kuchezesha mchezo wa UEFA Super Cup, hatua iliyomuweka kwenye historia ya mashindano hayo.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments