Kiswahili kinang'ara kupitia michezo Tanzania


Timothy Lugembe,

Mwanakwetusports.

Michezo imekuwa moja ya njia zinazowakutanisha watu kutoka mataifa tofauti tofauti , kwa Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zinazopokea wachezaji na mashabiki kutoka nje kwa ajili ya kushiriki au kufuatilia michezo mbalimbali, hasa mpira wa miguu.

Ujio wao nchini hauishii kwenye shughuli za uwanjani pekee bali Wanapokaa na wenyeji wao, hupata nafasi ya kujifunza tamaduni, mila na lugha inayotumiwa katika mazingira wanayoishi.

Lugha ya Kiswahili ni sehemu ya mawasiliano yao ya kila siku, Wachezaji kutoka nje wanapokuwa kambini, mazoezini au katika maisha ya kawaida, hujifunza maneno na misemo ya Kiswahili kutoka kwa wenzao. Mara nyingi mafunzo hayo huanzia kwenye mazungumzo, utani na vicheko, lakini baada ya muda maneno hayo huanza kuwa sehemu ya mawasiliano yao.

Mfano wa jambo hili unaonekana katika klabu ya Yanga, ambako mchezaji Denis Nkane amekuwa akimfundisha mwenzake Max Nzengeli ambaye ni raia wa Congo kuzungumza Kiswahili, Kupitia mawasiliano hayo, wamejenga urafiki na pia kuonyesha namna lugha inaweza kufundishwa ndani ya mazingira ya michezo.


Huo ni mfano mmoja tu lakini Jambo kama hili linaweza kutokea katika timu mbalimbali nchini, kwa sababu wachezaji wa kigeni huishi na kufanya kazi pamoja na Watanzania kwa muda mrefu, Kadiri wanavyojifunza Kiswahili, ndivyo wanavyoweza kuendelea kukitumia hata nje ya mazingira ya Tanzania.

Hata mashabiki wanaokuja nchini kwa ajili ya michezo hupata nafasi ya kukutana na utamaduni wa Tanzania, Wanapotembelea maeneo mbalimbali, kuzungumza na wenyeji na kushiriki shughuli za kijamii, Kiswahili huwa sehemu ya uzoefu wanaoondoka nao.

Kwa hiyo, mgeni anayekuja Tanzania kwa ajili ya michezo haondoki na kumbukumbu za mchezo pekee Bali anaweza pia kuondoka na maneno ya Kiswahili, utamaduni na uzoefu wa maisha ya Watanzania.

Michezo inaweza kuwa uwanja wa ushindani, lakini nje ya uwanja inaweza kuwa daraja la lugha na utamaduni. Kila mchezaji au shabiki anayejifunza na kutumia Kiswahili akiwa Tanzania anaongeza njia nyingine ya lugha hiyo kusikika nje ya mipaka ya Tanzania.

0767915473,

lugembetimothy01@gmail.com.



0/Post a Comment/Comments