Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Kwa miaka ya hivi karibuni, idadi ya watu wanaofanya jogging ( mazoezi ya kukimbia) imeongezeka katika miji na maeneo mbalimbali, Wapo wanaokimbia ili kuboresha afya, kupunguza uzito au kujiandaa kwa mashindano. Hata hivyo, wataalamu wa afya wanaeleza kuwa jogging ni zaidi ya mazoezi ya kawaida ni njia ya kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza na kuboresha afya ya akili.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu wazima wanapaswa kufanya angalau dakika 150 hadi 300 za mazoezi ya kiwango cha wastani kwa wiki, au dakika 75 hadi 150 za mazoezi ya nguvu zaidi na Jogging ni miongoni mwa mazoezi yanayoweza kumsaidia mtu kufikia kiwango hicho.
Kwa upande wa Madaktari wa moyo wanaeleza kuwa kukimbia mara kwa mara huongeza uwezo wa moyo kusukuma damu na kuboresha mzunguko wa damu mwilini, hali hiyo husaidia kupunguza hatari ya shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na kiharusi aidha, mwili hutumia nishati nyingi wakati wa kukimbia, jambo linalosaidia kudhibiti uzito unapounganishwa na lishe inayofaa.
Mbali na afya ya mwili, jogging ina mchango katika afya ya akili, American Psychological Association (APA) inaeleza kuwa mazoezi ya mwili yanaweza kupunguza msongo wa mawazo na kuboresha hali ya hisia. Wakati wa kukimbia, mwili hutoa kemikali zinazojulikana kama endorphins, ambazo huchangia kuongeza hali ya utulivu na kupunguza hisia za wasiwasi.
Tafiti pia zinaonyesha kuwa watu wanaofanya mazoezi mara kwa mara hupata usingizi wenye ubora zaidi, Kwa mujibu wa American Heart Association (AHA), mazoezi ya mwili yanapofanywa kwa utaratibu yanaweza kuboresha usingizi na kuongeza uwezo wa mwili kufanya shughuli za kila siku.
Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa jogging inapaswa kufanywa kwa utaratibua ambapo Wanaoanza wanashauriwa kuanza kwa kutembea kwa kasi, kisha kuongeza mwendo taratibu kadiri mwili unavyozoea Pia ni muhimu kufanya mazoezi ya kuandaa misuli kabla ya kukimbia, kuvaa viatu vinavyofaa na kunywa maji ya kutosha.
Kwa watu wenye matatizo ya moyo, viungo au magonjwa mengine ya muda mrefu, ushauri wa daktari ni muhimu kabla ya kuanza programu ya jogging. Hatua hiyo husaidia kuhakikisha mazoezi yanaendana na hali ya afya ya mhusika.
Kwa ujumla, ushahidi kutoka WHO na taasisi nyingine za afya unaonyesha kuwa jogging ni njia rahisi ya kuboresha afya ya mwili na akili pale inapofanywa kwa usahihi na kwa utaratibu, inaweza kupunguza hatari ya magonjwa, kuongeza nguvu za mwili na kusaidia mtu kuishi maisha yenye afya kwa muda mrefu
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.


Post a Comment