Timothy Lugembe,
Mwanakwetusports.
Jezi zimekuwa sehemu ya utambulisho wa mashabiki wa vilabu vya soka Tanzania na Duniani kwa ujumla, Kila msimu vilabu huingia sokoni na jezi mpya ambazo hutumiwa na mashabiki wakati wa michezo na katika shughuli nyingine za kijamii.
Hata hivyo, pamoja na kuendelea kubadilisha miundo ya jezi, bado kuna nafasi ya vilabu kuangalia mahitaji ya makundi tofauti ya mashabiki hasa wanawake.
Kwa sasa, vilabu vingi hutengeneza jezi kwa muundo unaolenga kutumiwa na mashabiki wote hali ambayo imefanya baadhi ya mashabiki wa kike kutumia ubunifu wao wenyewe kubadilisha namna jezi zinavyovaliwa.
Katika matukio ya soka Tanzania, baadhi ya wanawake wameonekana kukunja sehemu ya nyuma ya jezi zao ili kupata muundo wa "crop top", Mtindo huo umeonekana pia katika matamasha ya Simba na Yanga, ambapo mashabiki wa kike wamekuwa wakitumia jezi kwa namna hiyo.
Mwenendo huo unaweza kuwa ishara ya mahitaji ya aina nyingine za jezi katika soko la jezi Tanzania, badala ya mashabiki kubadilisha jezi walizonunua ili kupata muundo wanaoupenda, vilabu vinaweza kutengeneza matoleo maalumu yanayolenga wanawake.
Hatua hiyo inaweza kuifanya klabu kuwa na bidhaa zaidi sokoni mfano, pamoja na jezi za kawaida, klabu inaweza kuwa na jezi za wanawake zenye miundo tofauti kulingana na mahitaji ya wanunuzi.
Kwa upande wa biashara, kuongeza aina ya jezi kunaweza kuongeza idadi ya bidhaa zinazouzwa na hivyo kutoa nafasi ya kuongeza mapato ya klabu, hii ni kwa sababu mashabiki wanaweza kuwa na chaguo zaidi badala ya kutegemea aina moja ya jezi ambapo ubunifu huo huenda ukapendwa sio Tanzania tu mpaka nje ya mipaka.
Aidha, matamasha ya uzinduzi wa msimu yanaweza kutumika kama sehemu ya kukusanya maoni ya mashabiki kuhusu bidhaa wanazohitaji na kuyafanyia kazi kwa manufaa yao pia Vilabu vinaweza kuchunguza mitindo inayotumiwa na mashabiki na kuzingatia maoni hayo wakati wa kuandaa bidhaa za msimu unaofuata.
Hivyo, ubunifu wa jezi haupaswi kuishia kwenye kubadilisha rangi, michoro au kuweka nembo mpya bali unahitaji pia kuzingatia namna bidhaa inavyotumiwa na makundi mbalimbali ya mashabiki.
Kwa vilabu vya Tanzania, soko la mashabiki wa kike linaweza kuwa sehemu ya kuangaliwa katika kuongeza mapato kupitia bidhaa za klabu ikiwa mahitaji yao yatazingatiwa katika utengenezaji wa jezi, mashabiki watapata chaguo zaidi na klabu inaweza kupata soko jingine la bidhaa zake.
0767915473,
lugembetimothy01@gmail.com.





Post a Comment